Zambia inaomboleza kifo cha Rais Sata "King Cobra"
Rais Michael Sata wa Zambia aliyekuwa na umri wa miaka 77 amefariki dunia Jumanne
tarehe 28 Oktoba 2014 mjini London, alikokuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Mfalme
Edward VII. Marehemu Rais Sata aliondoka Zambia tarehe 19 Oktoba 2014 kuelekea London
kwa matibabu, huku akiwa amesindikizwa na familia yake.
Minong'ono kwamba,
Rais Sata alikuwa anaumwa sana ilianza kusikika kunako mwezi Juni, alipoweka hadharani
na kuelekea Israeli kupata matibabu. Mwezi Septemba alipangiwa kuhutubia kwenye Baraza
kuu la Umoja wa Mataifa, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na sababu za kiafya
na tangu wakati huo hakuweza kuonekana tena hadharani miongoni mwa wananchi wake.
Rais
Sata amefariki dunia wakati Zambia bado inasherehekea Jubilee ya miaka 50 tangu ilipojipatia
uhuru wake kutoka kwa Mwingereza. Zambia inatarajia kufanya uchaguzi mkuu katika kipindi
cha siku 90 kuanzia sasa.
Marehemu Rais Michael alizaliwa tarehe 6 Julai 1973
huko Mpika, Zambia. Baada ya kugombea urais kwa mara tano, hatimaye tarehe 23 Septemba
2011 akachaguliwa kuwaongoza wananchi wa Zambia. Alifahamika na wengi kwa jina la
utani "King Cobra", atakumbukwa na wengi kwa mikakati ya maendeleo endelevu kwa wananchi
wa Zambia. Waziri wa ulinzi Bwana Edgar Lungu anatarajiwa kuiongoza Serikali ya Zambia
katika kipindi hiki cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu.