Bwana Christos Stylianides, Mratibu mkuu wa ugonjwa wa Ebola kutoka Jumuiya ya Ulaya
anasema kwamba, kunahitajika jumla ya wataalam 40, 000 mapema iwezekanavyo ili kukabiliana
na janga la ugonjwa wa Ebola, huko Afrika Magharibi. Wataalam hawa wanapaswa kupewa
uhakika kwamba, wataweza kuondolewa katika maeneo watakayokuwa wanahudumia, kama hatari
ikijitokeza na kwamba, yeye mwenyewe atasimamia operesheni ya kuokoa wananchi wa Ulaya
ambao wameathirika kutokana na ugonjwa wa Ebola.
Bwana Stylianides anasema,
Jumuiya ya Kimataifa haikuchukua hatua madhubuti kupambana na ugonjwa wa Ebola kisayansi
tangu ulipojitokeza kwa mara ya kwanza na mapokeo yake, watu wakajikuta wanakumbatia
imani potofu. Serikali ya Marekani inaendelea kuchukua tahadhari kubwa kwa watu wanaotoka
katika maeneo ambayo yameathirika kwa ugonjwa wa Ebola, kwa kuwatenga kwa muda kabla
ya kuanza maisha ya kawaida katika familia zao.
Australia imeamua kusitisha
kutoa vibali vya kuingia nchini humo kwa wananchi wanaotoka katika nchi za Afrika
Magharibi kama sehemu ya tahadhari ya kuenea kwa ugonjwa wa Ebola.