2014-10-29 16:12:08

Kanisa si Mapadre au Maaskofu, bali wabatizwa wote


Baba Mtakatifu Francisco, katika mafundisho yake kwa mahujaji na wageni walio kusanyika katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro hapa Vatican, ameendelea kulizungumzia Kanisa, katika asili yake kuonekana na maana yake ya kiroho. Fumbo la mwili wa Kristo, uliojengwa ndani ya Roho Mtakatifu na pia uhalisi wa kanisa unao onekana kupitia jumuiya zake, Parokia na majimbo yake katika asili ya muundo wake wa kitaasisi wenye kuwaunganisha waumini kwa pamoja.

Papa amesema, uhalisi huu wa kuonekana wenyewe peke yake, ni fumbo linaonyesha upendo na fadhila nyingi za Mungu zilizofichika ndani mwake ambazo hutekelezwa na waumini wa Kanisa duniani kote. Na ili kuelewa uhusiano kati ya yale yanayoonekana na yale yanayofanyika katika kipimo cha kiroho ndani ya mwili wa Kristo, yaani Kanisa, tunahitaji kumtazama Yesu mwenyewe, kama Mungu na Mwanadamu.

Katika ubinadamu, Kristo anatimiza Mpango Mtakatifu wa Mungu wa kumkomboa binadamu. Na hivyo katika macho ya imani , tunaweza kuelewa jinsi Kanisa linavyo onekana katika mwelekeo wake wa kuzamisha ukweli kamili wa kiroho. Na kwa njia ya sakramenti zake na ushuhuda wake kwa Kristo, katika dunia yetu, Kanisa hutafuta kutangaza upendo wa Mungu na huruma yake kwa watu wote, hasa kwa maskini na wahitaji.

Katika mafundisho yake Papa, amesema, kwa mara nyingi tunasikia watu wakilalamikia Kanisa halijafanya hiki, halijafanya kile. Lakini, Papa akahoji , Kanisa ni nani hasa? , Je ni Mapadre au Maaskofu au Papa? Hapana , Kanisa ni wabatizwa wote. Waamini wote wa Kristo huunda Kanisa. Kanisa linaloonekana si tu la Mapadre, Maaskofu au Watawa, au Papa, bali ni mjumuiko wa waamini wote wabatizwa, wake kwa waume wa pande zote za dunia , ambao hutangaza kwa vitendo upendo wa Mungu usiokuwa na kipimo. Ni familia zilizo simama imara katika imani , ni wazazi wanaoieneza imani kwa watoto wao , ni wagonjwa wanao yatolea mateso yao kwa Bwana wa Kanisa. Huo ndiyo ulikuwa ujumbe wa Papa katika Katekesi hii.
Papa katika katekesi, amekiri uwepo wa udhaifu wa binadamu katika kanisa la kuonekana,udhaifu na mipaka ya kibinadamu, inayoweza kuliletea kanisa fedheha mbaya na hasa pale waumini wake wanapokuwa mfano mbaya au kuwa chimbuko la kashfa. Papa amesema wengi huumizwa na utendaji mbovu wa Mkristo kwa kuwa wengi hutegemea Wakristo kuwa mfano mzuri wa wema na utakatifu katika maisha. Hivyo pale Mkristo anapotenda kinyume na matarajio hayo, watu hukwazika, na pengine hata kanisa zima kulaumiwa, kama vile wote wametenda kosa hilo. Na hii inadhihirisha kila Mbatizwa kuwa sehemu ya mwili wa Kanisa, kuwa kiungo katika jumuiya wabatizwa, wote kama kanisa , Kanisa la Kristo.
Papa ametaja pia kwamba, Kanisa katika hali yake ya kuonekana, wafuasi wote wa Kristo, na katika jina la Kanisa, hujitahidi kuwa karibu na watu wote maskini na wale wanaoteseka, kwa ajili ya kutoa msaada, faraja na matumaini. Wote wanaofanya hivyo hufanya kwa ajili ya bwana aliyewatuma kama Kanisa. Na hivyo tunapata kuelewa kanisa katika maana ya uhalisi wake wa kuonekana kwa ajili ya mtazamo wake wa kina katika uhalisi wake wa kiroho.
Ombi kwa ajili ya wagonjwa wa ebola
Baada ya Katekesi, Papa ameonyesha kujali uwepo shambulio la ugonjwa wa ebola, na hivyo kurudia kutoa ombi lake, kwa jumuiya ya kimataifa kuchagiza zaidi juhudi za kupambana na virusi hivi. Alisema, Ili kukabiliana na janga la Ebola, alipenda kuelezea jinsi anavyo guswa na taarifa juu na ugonjwa huu unaonyimisha raha watu na hasa katika maeneo ulikoenea kwa kasi zaidi hasa katika mataifa kadha ya Afrika Magharibi. Papa pia ametaja makundi maalum yanayotoa huduma kwa watu wanaoshambuliwa na virusi hivyo, kama wauguzi, madaktari na watu wa kujitolea, ambao wanahatarisha maisha yao kwa ajili ya kuhudumia wengine.

Papa kwa moyo wa upendo, anatolea sala na maombi yake, kwa walioathirika, na wanaotoa huduma kama vile madaktari, manesi, wafanyakazi wa kujitolea, taasisi za dini na vyama, ambao wanafanya kazi kishujaa kuwasaidia ndugu na dada ambao ni wagonjwa wetu. Na hivyo kwa azma hiyo, alirudia kutoa upya ombi lake kwa jumuiya ya kimataifa, ifanya jitihada zote, kutokomeza virusi hivyo, na kupunguza matatizo na mateso ya wale ambao wamewekwa katika majaribu haya. Papa pia ametoa mwaliko kwa watu wote kuwakumbuka katika sala wale wote waliopoteza maisha yao kwa ugonjwa huu.







All the contents on this site are copyrighted ©.