Jimbo Katoliki la Mahenge, Tanzania, linaadhimisha kilele cha Jubilee ya miaka 50
tangu lilipoanzishwa kunako mwaka 1964 na Marehemu Askofu Elias Mchonde aliyekuwa
Askofu msaidizi wa Jimbo la Dar es Salaam akateuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo
Katoliki la Mahenge na kuliongoza Jimbo hili kuanzia wakati huo hadi mwaka 1969 alipofariki
dunia. Baadaye Jimbo limeongozwa na Askofu Nikas Kipengele tangu mwaka 1970 hadi mwaka
1971; Askofu Patrick Iteka kuanzia mwaka 1973 hadi mwaka 1993.
Askofu Agapiti
Ndorobo akapewa dhamana ya kuwaongoza waamini wa Jimbo Katoliki la Mahenge tangu mwaka
1995 hadi wakati huu, Jimbo linapomwimbie Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani na sifa
kwa kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya uwepo wake. Askofu Ndorobo ameliongoza Jimbo
kwa miaka 19 sasa. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha: mafanikio
na changamoto anazokabiliana nazo katika kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza
Watu wa Mungu Jimboni Mahenge.
Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la Ifakara
lililoanzishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2012 na Askofu
Salutaris Melchior Libena kuteuliw akuwa Askofu wake wa kwanza ni matunda ya Jimbo
Katoliki la Mahenge ambalo hapo awali lilikuwa na Parokia 38 lakini baada ya kuligawa
ili kurahisisha shughuli za kichungaji kwa Watu wa Mungu, sasa Jimbo Katoliki la Mahenge
lina Parokia 22, likiwa na waamini zaidi ya 215, 000 lakini hapo awali lilikuwa na
waamini 487, 000.
Askofu Ndorobo anasema kwamba, katika kipindi cha miaka 50
ya uwepo wa Jimbo Katoliki la Mahenge kumekuwepo na maendeleo makubwa katika medani
mbali mbali za maisha, lakini zaidi ni upendeleo kwa maskini na wale wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Kuna vituo vya kutunzia wagonjwa wa kifafa, kituo cha wagonjwa
wa Ukoma pamoja na kituo cha Watoto Yatima.
Jimbo Katoliki la Mahenge linamiliki
na kuendesha Sekondari 5; Vituo vya Afya na Zahanati 9 na kwamba kuna mpango mkakati
wa kuanzisha Hospitali ili kujibu kilio cha watu wenye shida na mahangaiko wanaolazimika
kutembea umbali mrefu ili kutafuta tiba kwa magonjwa yanayowasumbua, lengo ni kuendelea
kutangaza Injili ya Uhai, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu.
Askofu Ndorobo anakiri kwamba, Jimbo la Mahenge
limeendelea kuwa na miito mbali mbali ya maisha ya: Kipadre, Kitawa na Ndoa. Kuna
vyama vya miito vinavyosaidia mchakato wa malezi ya miito ndani ya Kanisa, kwa njia
ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, unaowachangamotisha vijana kupenda kushiriki katika
maisha ya Kipadre, Kitawa na Ndoa takatifu.
Askofu Ndorobo anasema miaka 19
ya utume wake kama Askofu wa Jimbo Katoliki Mahenge amekumbana na changamoto nyingi,
lakini katika mahojiano na Radio Vatican anagusia changamoto kuu mbili, yaani umuhimu
wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo na Maisha ya Sala na Kisakramenti. Anasema, kwa
miaka hii yote amependa kukazia umuhimu wa waamini kushiriki katika maisha ya Jumuiya
ndogo ndogo za Kikristo kwani hizi ni shule ya Sala, Neno la Mungu na kielelezo cha
imani tendaji.
Huu ndio mwelekeo ambao anapenda kuuendeleza hata baada ya
maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo Katoliki Mahenge. Anasema, amependa kukazia
umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika maisha ya Sala na Sakramenti za Kanisa
ili waweze kujichotea neema na baraka; waweze kuonja huruma na upendo kutoka kwa Mwenyezi
Mungu, tayari kufanya mabadiliko ya kina katika maisha yao, kwa ajili ya sifa na utukufu
wa Mungu. Viongozi wawe ni mfano bora wa maisha ya sala na Sakramenti za Kanisa, ili
wao wakiishaimarika, waweze pia kuwaimarisha ndugu zao katika imani, matumaini na
mapendo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.