Hija ya kichungaji ya Papa Francisko nchini Uturuki, inaonesha matumaini na ujasiri!
Kwa mara ya kwanza Mwenyeheri Paulo VI alitembelea nchini Uturuki kunako mwaka 1967
na Mtakatifu Yohane Paulo II akafanya hija ya kichungaji nchini humo kunako mwaka
1979 na kunako mwaka 2006 Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita akatembelea
tena Uturuki.
Kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 Novemba 2014, Baba Mtakatifu
Francisko atafanya hija ya kichungaji inayopania kuimarisha mchakato wa majadiliano
ya kiekumene, ili kukata mzizi wa mambo ambayo bado yanakwamisha umoja kamili kati
ya Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki.
Baba Mtakatifu anafanya hija hii
ya kichungaji wakati kuna hali tete ya usalama huko Mashariki ya Kati, ambako bado
vita, dhuluma na nyanyaso za kidini bado zinaendelea kusikika. Pamoja na hali hii
tete, lakini bado kuna ushahidi wa uwepo wa Wakristo katika eneo hili, kumbe, hija
ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mambo mengine, itasaidia kuwatia
moyo Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya Kati, ili kuendelea kushuhudia imani yao
kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya magumu wanayokabiliana nayo.
Padre Martin
Kmetec, Mkapuchini ambaye kwa miaka mingi anaishi nchini Uturuki anasema, lengo kubwa
la hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko ni kumtembelea ndugu yake katika
Kristo Patriaki Bartolomeo wa kwanza, ili kuendelea kuimarisha mchakato wa majadiliano
ya kiekumene ulioanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Historia ya
Makanisa nchini Uturuki bado inaonesha madonda makubwa na kwamba, kuna misigano ya
kidini inayoendelea kujitokeza.
Kuna njama za kutaka kuligeuza Kanisa kuu la
Mtakatifu Sofia kuwa tena Msikiti, hali ambayo inaweza kugumisha majadiliano na mahusiano
ya kidini nchini Uturuki. Hivi karibuni, Patriaki Bartolomeo wa kwanza alitoa mhadhara
kuhusu mchango wa Mtakatifu Yohane XXIII katika maisha na utume wa Kanisa, katika
mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox.
Mtakatifu Yohane XXIII alionesha dira na mwelekeo wa Kanisa kwa siku za usoni
na kwamba, Wakristo wanachangamotishwa kujikita katika hali ya unyenyekevu, ukweli
na uwazi, huku wakimwachia Roho Mtakatifu kuwasaidia kufikia lengo la umoja kamili.
Kanisa halina budi kusikitika kutokana na utengano ambao umedumu kwa kiasi kikubwa,
lakini linapaswa kuwa na ujasiri wa kuangalia mbele kwa imani na matumaini, kama walivyofanya
waasisi wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene, miaka hamsini iliyopita.
Kuanzia
tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014, Baba Mtakatifu Francisko alitembelea Yerusalemu,
kama kielelezo cha kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana, kuzungumza
na kusali na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu, hapo Baba Mtakatifu Francisko na
Patriaki Bartolomeo wa kwanza wakakutana pia na kusali pamoja, mwendelezo wa hija
ya majadiliano ya kiekumene, huku wakiongozwa na Roho Mtakatifu, ili kujenga na kuimarisha
umoja na mshikamano wa Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko anataka kuimarisha
mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili wote waweze kuwa wamoja kadiri ya mapenzi
ya Kristo mwenyewe. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kutembelea na kuzungumza na waamini
wa dini ya Kiislam, changamoto endelevu ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini
na kitamaduni kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, ili kweli amani, upendo,
mshikamano na mafao ya wengi yaweze kupewa kipaumbele cha kwanza anasema Padre Martin
Kmetec.