2014-10-28 10:54:14

Vietnam kuwekeza katika usafiri wa maji na teknolojia ya habari


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Hanoi asubuhi, Jumatatu, Oktoba 27, 2014 kuanza ziara rasmi ya siku mbili ya Kiserikali nchini Vietnam. Rais Kikwete amewasili mjini Hanoi akitokea nchi jirani ya Jamhuri ya Watu wa China ambako Jumapili, Oktoba 26, 2014 alimaliza ziara rasmi ya Kiserikali yeye mafaniko makubwa ya siku sita nchini humo.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Noi Bai mjini Hanoi, Rais Kikwete amepokelewa na viongozi wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam na baada ya mapumziko mafupi, Rais Kikwete amekwenda Kasri ya Kirais kukutana na Rais Truong Tan Sang kwa mazungumzo ya faragha na baadaye kwa mazungumzo ya Serikali kati ya Tanzania na Vietnam.

Mara baada ya kuwasili kwenye Kasri hiyo, Rais alipokelewa na Rais Sang na akakagua gwaride la heshima ambalo liliundwa na Jeshi la nchi hiyo lililokuwa na vikosi vya anga, maji na nchi kavu.

Baada ya mazungumzo hayo, Marais hao wawili wameshuhudia utiaji saini wa Makubaliano katika Usafiri wa Majini (Marine Transport) ambao umetiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe kwa niaba ya Tanzania na Waziri wa Usafirishaji wa Vietnam, Mheshimiwa Dinh Li Thang kwa niaba ya nchi yake.

Mbali na kukutana na Rais Sang, Rais Kikwete baadaye amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam, Mheshimiwa Nguyen Phu Trong, ambaye pia ndiye kiongozi mkuu wa nchi hiyo. Viongozi hao wawili wamekutana kwenye Makao Makuu ya Kamati Kuu ya Chama hicho cha Kikomunisti, yanayoangaliana na Kasri ya Rais.

Rais Kikwete pia amefanya ziara kwenye Makao Makuu ya Kampuni ya Simu ya Viettel ambayo inajiandaa kuingia katika soko la vijijini katika Tanzania. Wakati wa mazungumzo kati ya Rais Kikwete na viongozi wa Kampuni hiyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Juliet Kairuki ameukabidhi uongozi wa Kampuni hiyo hati ya kuanzishwa kwa Kituo hicho.

Baadaye usiku, Rais Kikwete amehudhuria Hafla ya Chakula cha Jioni iliyoandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Rais Sang kwenye Kituo cha Kimataifa cha International Convention Centre mjini Hanoi. Rais Kikwete ataendelea na ziara yake ya Vietnam leo kwa kutembelea sehemu mbali mbali na kukutana na Spika wa Bunge la Vietnam, Mheshimiwa Nguyen Sinh Hung.

Hiyo ni ziara ya kwanza kufanywa na Mheshimiwa Kikwete akiwa Rais wa Tanzania, lakini hiyo ni mara ya pili kwake kutembelea Vietnam. Alitembelea Vietnam mwaka 2004, akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Wakati huo huo habari zinasema kwamba, kila Mtanzania nchini atakuwa na uwezo wa kupata simu ya kisasa na yenye uwezo mkubwa (smart phone) kwa bei ya chini kabisa katika miaka mitano ijayo kuanzia mwaka 2020 kwa mujibu wa mipango ya kampuni mpya ya simu inayojiandaa kuingia katika soko la simu la Tanzania.
Aidha, Kampuni ya Viettel ya Vietnam imemwambia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatatu, Oktoba 27, mwaka huu, 2014 kuwa itateremsha kwa kiasi kikubwa bei ya simu za kawaida na smart phone, ili kuwezesha kila Mtanzania kuwa na simu.

Kampuni hiyo pia imemwambia Rais Kikwete kuwa itasambaza mawasiliano ya internet kwa kila kijiji nchini na kuwa kwa taasisi za umma kama vile shule, hospitali, vituo vya polisi zitapatiwa huduma hiyo bila malipo yoyote. Rais Kikwete ameambiwa habari hiyo njema kwa Watanzania na Mwenyekiti wa Kampuni ya Simu ya Viettel wakati alipotembelea makao makuu ya Kampuni hiyo mjini Hanoi kwenye siku yake ya kwanza ya ziara yake rasmi ya Kiserikali katika Vietnam.

Mwenyekiti wa Kampuni hiyo ya umma ambayo inamilikiwa na Jeshi la Vietnam, Bwana Nguyen Manh Hung amemwambia Rais Kikwete kuwa Viettel inakusudia kumwezesha kila Mtanzania kumiliki smart phone kwa kupunguza bei ya simu hiyo na pia kupunguza bei ya huduma muhimu kama vile ile ya internet.

Bwana Hung amesema kuwa Kampuni yake inapanga kupunguza bei ya simu za kawaida hadi kufikia dola za Marekani 15, sawa na shilingi 25,000 na punguza ile bei ya smart phone hadi kufikia dola za Marekani 40, sawa na shilingi 65,000. Sasa hivi, bei ya simu hizo ni kubwa mara nyingi ya kisai hicho kinachokusudiwa.

“Tunataka kuifanya bei ya kununua smart phone kuwa mara 10 chini ya bei ya kununua kompyuta. Tunasukudia pia kupunguza bei ya matumizi ya simu kuwa dola moja tu ya Marekani, sawa na shilingi 1,600, kwa watu wa kawaida kwa mwezi na kwa wale ambao wanatumia simu kwa huduma nyingi zaidi watalipa dola za Merakani 50, sawa na shilingi 78,000, kwa mwezi,” amesema Bwana Hung.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa Kampuni yake itawekeza kiasi cha dola za Marekani bilioni moja katika huduma za simu na huduma nyingine katika Tanzania na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya pili nyuma ya Peru kupata mfumo wa simu wa kisasa zaidi miongoni mwa nchi ambako Kampuni hiyo ina shughuli zake.

Amesema kuwa ndani ya miaka mitatu tokea Kampuni hiyo kuanza shughuli zake katika Tanzania, kiasi cha vijiji 4,000 ambavyo kwa sasa havina mawasiliano vitapatiwa huduma hiyo katika awamu ya kwanza.

“Katika awamu ya pili, kiasi cha vituo 150 vya polisi, hospitali za umma 150, ofisi za Shirika la Posta kiasi cha 65 nchini vitapatiwa huduma ya mawasiliamo yakiwemo ya internet bure katika mwaka wa kwanza wa Kampuni hiyo kuanza shughuli zake. Tutatoa pia huduma ya internet na mfumo wa teknolojia ya mawasiliano bure kwa shule 450 za umma katika wilaya 150 ambazo tayari zina umeme, huduma ambazo pia zitatolewa katika mwaka wa kwanza wa Kampuni hiyo kuanza kazi,”amesema.

Bwana Hung amesema kuwa Kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka 1989 iliingia katika shughuli za simu mwaka 2000 na kuanza shughuli za simu za mkononi mwaka 2004.Mwaka 2013, mapato ya kampuni hiyo yalikuwa ni dola za Marekani bilioni 9.1 na kati ya hizo kampuni hiyo ilikuwa imepata faida ya karibu dola za Marekani bilioni moja.








All the contents on this site are copyrighted ©.