Amani na utulivu ni vichocheo vya maendeleo endelevu!
Kwa mara ya kwanza Rais Yoweri Kaguta Museveni alitembelea na kuzungumza na waandishi
wa habari wa Radio Vatican kunako mwaka 2001 na tarehe 27 Oktoba 2014 mara baada ya
kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican alitembelea tena Radio Vatican
na kuzungumzia kwa namna ya pekee mchango wa dini katika ustawi na maendeleo ya wananchi
wa Uganda; uwekezaji, amani na usalama; usalama wa chakula Uganda pamoja na maandalizi
ya uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika nchini Uganda kunako mwaka 2015.
Rais
Museveni anasema, kimsingi Waganda kama walivyo watu wengi Barani Afrika walikuwa
na imani zao za jadi, lakini ujio wa Wakristo na Waislam, ulileta mwelekeo mpya kuhusiana
na uelewa wa Mwenyezi Mungu kama Muumbaji na maisha baada ya kifo. Dini zimechangia
kwa kiasi kikubwa dhana ya msamaha na upatanisho badala ya kulipizana kisasi pamoja
na mapendo kwa Mungu na jirani; tunu msingi katika maisha ya kiroho kwa kila mwamini.
Serikali ya Uganda inaheshimu uhuru wa kuabudu.
Rais Museveni anasema kwamba,
Kanisa Katoliki limechangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya wananchi
wa Uganda katika sekta ya elimu, afya, maji na maendeleo endelevu, kiasi kwamba, wananchi
wa Uganda wanaendelea kucharuka katika maboresho ya maisha yao ya kila siku.
Serikali
ya Uganda inaendelea kuwaalika wawekezaji kutoka ndani na nje ya Uganda ili kuwekeza
katika sekta ya miundo mbinu, nishati, usafiri, kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa,
bila kusahau utalii na uzalishaji wa bidhaa viwandani. Uganda itaendelea kuweka mazingira
bora kwa wawekezaji na kwamba, hakuna anayebaguliwa, bali jambo la msingi ni kuhakikisha
kwamba, kila mwekezaji awe ni wa ndani au wa nje anafuata sheria na kanuni msingi
zilizowekwa.
Rais Museveni anasema, Uganda itaendelea kusaidia mchakato wa
upatikanaji wa amani na utulivu katika nchi za Afrika Mashariki, kwa kushiriki katika
mikakati ya ulinzi na usalama. Lengo ni kuhakikisha kwamba, amani inapatikana kwa
wote na kwamba hiki ni kichocheo kikubwa cha ustawi na maendeleo ya watu wa Bara la
Afrika.
Rais Museveni akizungumzia kuhusu mikakati ya kuwa na uhakika wa usalama
wa chakula nchini Uganda anasema, kimsingi Uganda imebahatika kuwa na ardhi yenye
rutuba nzuri na vyanzo vingi vya maji na kwamba, kwa miaka mingi Waganda wamejielekeza
katika sekta ya kilimo na kwamba, Uganda ina chakula cha kutosha. Jambo la msingi
ni wananchi kujifunza sasa kula lishe bora kwa ajili ya afya zao. Uhakika wa usalama
wa chakula unachangiwa na uwezo wa watu kununua chakula kilichopo sokoni. Wananchi
wa Uganda wana uwezo wa kujinunulia chakula kwa wakati huu.
Rais Museveni katika
mahojiano na Radio Vatican anabainisha kwamba, kwa sasa Serikali yake inaendelea kujiandaa
kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo mwakani kwa: kujikita
katika utoaji wa huduma bora; kwa kuwekeza katika miundo mbinu; amani na utulivu pamoja
na kujitegemea. Anasema Serikali yake inapenda kutambulikwa kwa vitendo na wala si
kwa maneno matupu na kwamba, uchaguzi mkuu ni majumuisho ya mikakati yote hii inayopania
ustawi na maendeleo ya wananchi wa Uganda.