Zawadi ya maisha, utu na heshima ya binadamu ni mambo msingi katika kukuza amani!
Kongamano la Kimataifa la siku mbili lililoandaliwa na Mfuko wa Josefu Ratzinger na
kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya elfu moja kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Medellin,
nchini Colombia, kwa kuongozwa na kauli mbiu, “heshima kwa zawadi ya maisha ni njia
ya amani” lilipata baraka ya ujumbe kutoka kwa viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki.
Baba
Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin,
Katibu mkuu wa Vatican, amewataka washiriki wa kongamano hili la kimataifa kuzingatia
kwa makini Mafundisho ya Kanisa yanayokazia umuhimu wa kulinda, kutunza na kudumisha
zawadi ya maisha, kama kiungo muhimu sana cha amani duniani. Hii ni dhamana inayopaswa
kumwilishwa katika mioyo ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema.
Baba Mtakatifu
anasema, utandawazi unaufanya ulimwengu kuwa kama kijiji, lakini kwa bahati mbaya
watu hawawezi kuishi kwa umoja na mshikamano kama ndugu na matokeo yake, kinzani na
migogoro ya kijamii inazidi kushamiri siku hadi siku. Baba Mtakatifu anawaalika waamini
na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, kuchuchumilia
mafao ya wengi sanjari na kuheshimu utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu; mambo msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu na mshikamano na wote.
Papa
Mstaafu Benedikto XVI katika ujumbe wake kwa washiriki wa kongamano hili la kimataifa
anasema kwamba, ni tukio ambalo limejitahidi kusoma alama za nyakati kwa kuangalia
matatizo na changamoto zinazowakabili walimwengu kwa sasa. Kutafuta, kulinda na kudumisha
amani ni changamoto endelevu kwa nyakati hizi kutokana na ukweli kwamba, kuna maeneo
mengi ya dunia ambamo vita inazidi kusababisha vifo na majanga mbali mbali.
Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI anasema, imani kwa Mwenyezi Mungu, Muumba wa vyote
ni msingi unaomsukuma mwanadamu kulinda na kutetea maisha, utu na heshima ya binadamu
aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hii ni haki yake msingi. Amani na utu wa mwanadamu
ni mambo ambayo yanapata msingi wake katika imani kwa Mwenyezi Mungu.
Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI amekumbusha kwamba, mara baada ya maadhimisho ya
Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Mababa wa Kanisa kutoka katika Nchi za Amerika ya
Kusini, walikusanyika kwa mara ya kwanza huko Medellin; mkutano ambao ulizinduliwa
na Mwenyeheri Paulo VI aliyewatakia amani ya kweli inayopata chimbuko lake kutoka
katika moyo wa mwanadamu; amani inayokazia msingi wa haki na mshikamano mintarafu
mwanga wa Injili. Amani ni changamoto kubwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu
kwa siku za usoni.