Rais Yoweri Museveni wa Uganda akutana na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 27 Oktoba 2014 amekutana na kuzungumza na
Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda pamoja na msafara wake, uliomtembelea mjini
Vatican. Baadaye, Rais Museveni amefanya mazungumzo na Kardinali Pietro Parolin, Katibu
mkuu wa Vatican aliyekua ameambatana na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu
wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican
Baba Mtakatifu
na Rais Museveni wamejadili kwa kina na mapana hali ya maisha ya wanachi wa Uganda
pamoja na kuonesha uhusiano mwema uliopo kati ya Serikali ya Uganda, Vatican na Kanisa
kwa ujumla, hasa kwa Kanisa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu, afya
na maendeleo endelevu ya watu. Viongozi hawa wamekazia umuhimu wa watu kuheshimiana
na kuthaminiana huku wakiishi kwa amani na utulivu.
Mwishoni, Baba Mtakatifu
na Rais Museveni wamegusia pia masuala ya kimataifa, lakini kwa namna ya pekee, maeneo
ya Bara la Afrika ambayo kwa sasa yanakabiliana na vita pamoja na kinzani za kijamii.