2014-10-25 14:59:11

Utu wa binadamu ni kanuni msingi kwa ajili ya mikakati ya maendeleo endelevu!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Ijumaa tarehe 24 Oktoba 2014 ameshiriki katika mkutano kuhusu utu wa binadamu na maendeleo ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Notre Dame Global Gateway, kilichoko mjini Roma; mkutano ambao ulifunguliwa rasmi hapo tarehe 22 Oktoba 2014. Katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huu, Kardinali Parolin amekazia umuhimu wa utu na heshima ya binadamu kama anavyoendelea kuhimiza Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho yake.

Maendeleo ya binadamu hayana budi kwenda sanjari na matumizi sahihi ya rasilimali, ili kuleta maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili. Ili kufikia lengo hili, mwanadamu hana budi kuwa ni kiini cha mipango na mikakati yote maendeleo, vinginevyo utu na heshima ya binadamu vitakuwa hatarini. Hapa kuna haja ya kuongozwa na kanuni maadili na mshikamano wa kidugu, ili kusikiliza kilio na mahangaiko ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, vinginevyo kuna hatari ya kujenga utamaduni wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu, utandawazi unaojikita katika ubinafsi.

Kardinali Parolin anakumbusha kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; akakombolewa na Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, ili kumwezesha kuwa na mwelekeo wa maisha mapya yanayojikita katika misingi ya haki na amani, kwa kutambua kwamba, Mungu ni upendo. Walimwengu wajifunze kujenga na kudumisha uhuru unaotambua mafao ya wengi pamoja na ukuu wa Mungu kwa kujikita katika kanuni maadili.

Maendeleo yanaweza kupatikana ikiwa kama watu watajitahidi kuwa wema na waadili, wakweli na wanyofu katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati yo ya kiuchumi, kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi. Mikakati bora ya kiuchumi inahitaji toba na wongofu wa ndani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.