Kanisa linamshukuru Mungu kwa zawadi ya Askofu Josefu Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma
Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba ambaye pia ni msimamizi wa kitume
wa Jimbo Katoliki Singida, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema anapenda
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwajalia waamini wa Jimbo Katoliki la Kigoma mchungaji
mkuu atakayewaongoza, wafundisha na kuwatakatifuza kadiri ya mapenzi ya Mungu.
Anamshukuru
Baba Mtakatifu Francisko kwa kumteua Askofu Josefu Mlola, kwani hii inaonesha kwamba,
ana mpango naye kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu Jimboni Kigoma.
Hii ni neema na baraka ambayo waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuifurahia
kwani hiki ni chombo cha Mungu kwa ajili ya kazi ya ukombozi. Kama kiongozi ana mapaji,
karama na mapungufu yake, lakini Mungu amemwona kuwa ndiye anayehitaji kuliongoza
Jimbo Katoliki la Kigoma.
Askofu Rwoma anawaalika watu kuendelea kumpongeza
kwa njia ya sala pamoja na kumshika mkono, ili kazi hii mpya iweze kuzaa matunda ya
toba, wongofu wa ndani na maendeleo kwa wananchi wa Kigoma katika ujumla wao.