Jamhuri ya Watu wa China Ijumaa, Oktoba 24, 2014, imetangaza neema kubwa kwa Tanzania,
ikiwa ni pamoja na kutoa dola za Marekani milioni 85 kwa ajili ya shughuli za maendeleo
na kuisaidia Tanzania kufanya mageuzi ya viwanda. Neema hiyo ya China kwa Tanzania
imetangazwa na Rais Xi Jinping wa nchi hiyo katika mazungumzo rasmi ya Kiserikali
kati yake na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye yuko katika ziara rasmi ya siku sita katika
China.
Mazungumzo hayo kwenye Jumba la The Great Hall of the People yamefanyika
baada ya Rais Kikwete kukaribishwa rasmi katika Jamhuri ya Watu wa China kwa kupokelewa
na Rais Xi Jinping katika eneo la East Plaza ya Jumba hilo. Katika mapokezi hayo ya
kuvutia na kusisimua, Rais Kikwete amepigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride la ukakamavu
la Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China la People’s Liberation Army.
Katika
mazungumzo hayo, Rais Xi Jinping alitangaza kuwa China itaipatia Tanzania kiasi cha
dola milioni 85 ikiwa ni mchanganyiko wa msaada na mkopo usiokuwa na riba, fedha ambazo
Tanzania itaamua yenyewe jinsi gani ya kuzitumia. “Katika kuunga mkono jitihada za
Serikali ya Tanzania kuboresha maisha ya wananchi wake, napenda kutangaza kuwa Jamhuri
ya Watu wa China itatoa kiasi cha RMB milioni 200 ikiwa ni msaada na RMB 200 milioni
nyingine zikiwa ni mkopo usiokuwa na riba kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na kiasi cha RMB 100 milioni za msaada kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambazo
zitatumika kwa kadri Serikali hizo mbili zitakavyoamua,” amesema Rais Jinping.
Rais
huyo wa China pia ametangaza kuwa nchi hiyo itaisaidia Tanzania katika uendelezaji
wa maeneo ya uwekezaji ya EPZ, uendelezaji wa miundombinu, itaharakisha ujenzi wa
Bandari ya Bagamoyo na itaingia katika shughuli za kutafuta gesi na mafuta katika
ukanda wa Bahari ya Hindi katika eneo la Tanzania.
Rais Jinping pia ametangaza
kuwa Serikali ya China imefanya uamuzi wa kuikarabati Reli ya Uhuru ya TAZARA inayounganisha
Tanzania na Zambia na yenye urefu wa kilomita 1,860 na kusaidia uendeshaji wa reli
hiyo. “Ili kutekeleza uamuzi huu kwa haraka, napendekeza kuundwa kwa kamati ya pamoja
ya wataalam kuandaa ramani ya namna ya kuitoa reli hiyo katika matatizo yake ya sasa.”
TAZARA ndiyo reli ya kwanza duniani kujengwa na Jamhuri ya Watu wa China ambao utaalamu
wake sasa unasakwa na nchi nyingine nyingi duniani.
Rais Jinping pia ametangaza
kuwa Serikali yake itatoa nafasi 100 za masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi kutoka
Tanzania katika miaka mitano ijayo, itaongeza idadi ya madaktari ambao China inapeleka
Tanzania, itahimiza makampuni zaidi ya China kuwekeza katika Uchumi wa Tanzania na
kuzishawishi taasisi za kifedha za China kuanzisha shughuli zake nchini Tanzania.
Kiongozi
huyo wa China pia ametangaza kuwa nchi yake itajenga chuo kikubwa cha mafunzo ya ufundi
katika Tanzania na itaendelea kushirikiana na Tanzania katika eneo la uimarishaji
wa ulinzi na usalama. Rais Jinping amesema kuwa urafiki na uhusiano kati ya China
na Tanzania ni mfano unaong’ara wa uhusiano mzuri na mwema duniani na kuwa China iko
tayari kutoa uzoefu wake wa maendeleo kwa Tanzania bila wasiwasi wowote.
Rais
Kikwete amemshukuru sana Rais Jinping na Jamhuri ya Watu wa China kwa misaada yake
ambayo baadhi yake haikutarajiwa.