Waonjesheni wengine fadhila ya upendo inayojikita katika unyenyekevu, ufukara na furaha
ya kweli!
Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa
wenyeheri na watakatifu, Jumamosi, tarehe 25 Oktoba 2014 anatarajiwa kumtangaza Mtumishi
wa Mungu Sr. Assunta Marchetti kuwa Mwenyeheri, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa
huko San Paolo, Brazil. Mwenyeheri Sr. Assunta Marchetti alizaliwa kunako mwaka 1871
huko Lucca, Kaskazini mwa Italia, akiwa ni mtoto wa tatu kati ya watoto kumi na moja
katika familia ambayo ilibahatika pia kuwa na Padre aliyejulikana kwa jina la Padre
Giuseppe Marchetti.
Sr. Assunta ni mwanamke wa shoka aliyejipambanua kwa huduma
makini kwa watoto maskini waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi,
maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwa kuanzisha Kituo cha
Watoto Yatima huko San Paolo, Brazil. Sr. Assunta alijishughulisha kwa kiasi kikubwa
na huduma kwa maskini, yatima na wagonjwa, lakini baada ya kushikwa na ugonjwa, afya
yake ilianza kudorora na hatimaye, akiwa na umri wa miaka 77 akifariki dunia, kunako
tarehe 1 Julai 1948.
Sr. Assunta alionesha fadhila ya upendo, akaguswa na mahangaiko
ya watoto maskini, kiasi hata cha kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza, akiwaonesha
na kuwaonjesha watoto hao, upendo wa kimama. Alishuhudia imani yake katika matendo,
daima akitegemea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Aliwafundisha watoto
kusali na kumtegemea Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani anasema Kardinali
Angelo Amato, kiasi kwamba, shughuli hizi za kimissionari zikaacha chapa ya kudumu
katika maisha na utume wake nchini Brazil Aliwaonjesha watoto ukarimu wa mapendo,
daima akitambua na kuiona ile sura ya Kristo mteswa katika nyuso za watoto wadogo,
akapendwa na kuheshimiwa sana na watu kutoka ndani na nje ya Jimbo la San Paulo, Brazil.
Mwenyeheri
Sr. Assunta Marchetti ameliachia Kanisa urithi mkubwa wa kutambua kwamba, upendo wa
kimama ni huduma inayojikita katika unyenyekevu, sadaka na uvumilivu. Huu ni mwaliko
anasema Kardinali Angelo Amato kwa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha
fadhila ya upendo inayojikita katika unyenyekevu, ufukara na furaha ya kweli.