Wakristo wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwani
huu ni mwaliko na wito kwa wote na wala si kwa kundi la watu wachache ndani ya Kanisa.
Changamoto hii imetiliwa mkazo kwa namna ya pekee kabisa na Mababa wa Mtaguso mkuu
wa Pili wa Vatican, ili kuwawezesha Wakristo kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga
wa mataifa. Lengo ni kuyatakatifuza malimwengu.
Mtakatifu
Paulo Mtume anapoawaandikia Wakorintho: 1 Kor. 1: 1-2 anawakumbusha kwamba wao wametakatifuzwa
kwa njia ya Yesu Kristo, katika: maji na Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Sakramenti ya
Ubatizo, Wakristo wanafanyika kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa,
wakiwa na haki na wajibu unaoambatana na wito huu. Kwa njia ya Ubatizo, Wakristo wanauvua
utu wa kale uliochakaa kwa njia ya dhambi na kuanza kujivika utu mpya na kutembea
katika mwanga wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.
Mtume
Paulo katika nyaraka zake anatumia neno “Mtakatifu” kuwaelezea wale waliozaliwa kwa
maji na Roho Mtakatifu, yaani, wafuasi wa Kristo. Kumbe, Sakramenti ya Ubatizo inawapatia
waamini neema ya utakaso kwa kuwaondolea ile dhambi ya asili. Ni wajibu na jukumu
lao kuendelea kuitunza neema ya utakaso waliyoipokea kwa njia ya maisha adili yanayorutubishwa
kwa njia ya: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma, kielelezo
makini cha imani katika matendo.
Kwa njia ya Ubatizo, Wakristo wametengwa na
dhambi na hivyo kuunganishwa na Kristo ambaye ni: njia, ukweli na uzima. Kumbe, Wakristo
wanapaswa kuchangamkia utakatifu wa maisha kama sehemu ya mchakato endelevu wa maisha
yao. Hii ni safari ndefu inayojikita katika uhalisia wa maisha ya kila siku na kwamba,
kila mwamini akitaka na kuinua anaweza kuwa mtakatifu kwani huu ni mwaliko na wito
kwa wote, jaribu, utagundua siri ya mafanikio.
Na Padre Richard Mjigwa, C.PP.
S., Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.