2014-10-24 14:25:42

Upendo na ukweli vivunjilie mbali vizingiti vinavyokwamisha umoja wa Kanisa


Wanachama wa Mfuko wa "Orientale Lumen" unaosimamiwa na Askofu mkuu Kallistos wa Jimbo kuu la Diokleia wanaendelea na hija ya maisha ya kiroho mjini Roma kama sehemu ya mchakato wa kutaka kufanya maboresho katika maisha yao ya kiroho, kwa kushikamana zaidi na Yesu, chimbuko la imani na mlango wa utimilifu wao. Ni hija inayojielekeza katika mchakato wa upatanisho, ili kujenga na kuimarisha umoja kamili kati ya Wakristo.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na wajumbe hawa siku ya Ijumaa tarehe 24 Oktoba 2014 mjini Vatican amekumbusha kwamba, hakuna majadiliano ya kweli ya kiekumene yasiyojikita katika dhamana ya mabadiliko ya ndani sanjari na kuhakikisha kwamba, waamini wanakuwa waaminifu kwa Kristo pamoja na kutekeleza mapenzi yake.

Baba Mtakatifu amewapongeza wajumbe hawa kwa hija hii ambayo pamoja na mambo mengine inapenda kuwakumbuka kwa namna ya pekee Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II, waliotangazwa na Mama Kanisa, Aprili, 2013; viongozi waliojielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na Makanisa ya Kiorthodox kutoka Mashariki. Ni viongozi ambao wameonesha ari na moyo wa kutaka kukuza na kudumisha umoja miongoni mwa Wakristo, ili wote waweze kuwa wamoja chini ya Kristo.

Mtakatifu Yohane XXIII alipokuwa anatangaza nia yake ya kuitisha Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, alipania kuona umoja miongoni mwa Wakristo, dhamana iliyoendelezwa kwa ari kubwa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kama inavyojidhihirisha katika Waraka wake wa Kichungaji, Ut Unum Sint, "Ili Wote Wawe Wamoja".

Baba Mtakatifu amewaomba wajumbe hao wakati wa hija yao ya kitume mjini Roma kumkumbuka katika sala zao, ili aweze kutekeleza dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa ajili ya huduma ya mshikamano na umoja ndani ya Kanisa kwa kufuata mapenzi ya Kristo mwenyewe.

Baba Mtakatifu Francisko amewataka pia kumfikishia salam na matashi mema Patriaki Bartolomeo wa kwanza watakapomtembelea na kukumbusha kwamba, hata Yeye mwenyewe amekubali mwaliko na kwa sasa anajiandaa kwenda kumtembelea ili kwa pamoja waweze kuadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Andrea, kama kielelezo makini cha umoja na mshikamano kati ya Roma na Costantinopoli, ili kuvunjilia mbali kwa njia ya upendo na ukweli vizingiti ambavyo vinakwamisha umoja wa Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.