Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amewasili nchini Poland kwa ziara ya siku mbili
ya Kiserikali ambayo inalenga kuwavutia wafanyabiashara wa nchi hii waje kuwekeza
Tanzania. Mara baada ya kuwasili jijini Warsaw, akitokea London Uingereza, Waziri
Mkuu Alhamisi, Oktoba 23, 2014) alikutana na wafanyabiashara zaidi ya 50 kwenye mkutano
uliofanyika kwenye ofisi za Chama cha Wafanyabiashara cha Poland (Polish Chamber of
Commerce). Katika Mkutano huo, Waziri Mkuu aliwaeleza mipango ya Serikali ya kuikwamua
Tanzania kiuchumi huku akigusia sekta za kilimo, uvuvi, uchukuzi, miundombinu, madini,
nishati na utalii. “Nia ya ziara yangu fupi lakini yenye malengo mahsusi ni kuamsha
mahusiano baina ya nchi zetu mbili lakini zaidi ni kutafuta mbinu za kukuza biashara
kati ya Tanzania na Poland. Nataka muione Tanzania kama mahali salama pa kuwekeza
mitaji yenu, mahali rafiki pa kuweka mitaji lakini pia mahali pa kufanya biashara
ambayo pia itahusisha uwekezaji,”alisema. Katika mkutano huo Waziri Mkuu alijibu
maswali kutoka kwa wafanyabiashara zaidi ya 10 ambao walikuwa na shauku ya kutaka
kufahamu ni maeneo yapi zaidi yanayohitaji uwekezaji. Pia aliishukuru Serikali
ya Poland kwa kusaidia ukarabati na uimarishaji wa miundombinu kwenye Chuo cha Maendeleo
ya Jamii cha Tengeru, kilichopo Arusha. Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuongea
na wafanyabiashara hao, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland anayeshughulikia masuala
ya Afrika na Mashariki ya Kati, Bibi Katarzyna Kacperczyk alisema nchi hiyo imeanzisha
mpango maalum ujulikanao kama “Go Africa” ambao umelenga kukuza mahusiano ya kiuchumi
na bara la Afrika. “Tukiwa ndani ya Jumuiya ya Ulaya, pamoja na hatua kubwa za
kiuchumi tunazokwenda nazo, kama Serikali tuliamua kwa dhati kwamba hatuwezi kuwaacha
ndugu wetu wa iliyokuwa Ulaya Mashariki kabla ya mageuzi ya kiuchumi duniani... lakini
tumeamua kuangalia bara la Afrika kama mdau muhimu wa maendeleo lakini pia kama soko
la uhakika kwa bidhaa tunazozalisha,”alisema. Alisema mpango huo umeanzisha mahsusi
ili kuwasaidia wafantabiashara wa Poland kupata taarifa sahihi na haraka kuhusiana
na masuala ya ushirikiano na uwekezaji barani humo. Alisema wameanzisha mpango
huo ili kuwahamasisha wenye makampuni barani Afrika waone kuna wenzao wa Poland na
waamue kushirikiana katika kulijenga bara la Afrika. Waziri Mkuu leo atatembelea
kampuni ya Rol Brat inayotengeza zana za kisasa za kilimo yakiwemo matrekta na mashine
za kuvuna mazao mazao mashambani. Pia atatembelea kampuni ya “Mtynpol” ambayo inahusika
na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia vyakula na miundombinu yake.