2014-10-24 11:39:01

Kanisa la Kristo linajwengwa kwa matofali ya: unyenyekevu, upole na kuchukuliana kwa upendo ili kudumisha umoja!


Kila Mkristo anachangamotishwa na Mama Kanisa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kwa kumwachia Roho Mtakatifu, aweze kuliongoza na kuimarisha umoja wa Kanisa unaojikita katika tofauti zinazojionesha katika watu. Mwaliko huu ulitolewa kwa mara kwanza na Mtakatifu Paulo na Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Siku ya Ijumaa ameukazia ujumbe huu, akikumbusha kwamba, hii ni dhamana endelevu kwa Wakristo wa nyakati zote.

Mtakatifu Petro anazungumzia kuhusu Kanisa lililojengwa kwa mawe, ambalo kila Mkristo anashiriki kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, lakini waamini watambue kwamba, wanapaswa kujiepusha na kiburi kama walivyoonesha Waisraeli wakati wa ujenzi wa Mnara wa Babeli, hapo wakaiona hasira ya Mungu ikiwaka juu yao na kusambaratika katika uso wa dunia kama umande wa asubuhi. Mnara wa Babeli ni kielelezo cha utengano kati ya binadamu, lakini Kanisa la Kristo linapaswa kuwa ni kielelezo makini cha umoja unaojionesha hata katika tofauti.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu Kristo ndiye jiwe kuu la msingi katika ujenzi wa umoja na mshikamano ndani ya Kanisa na kwamba, Yesu mwenyewe siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alimwomba Baba yake wa Mbinguni ili wanafunzi wake waweze kuwa wamoja, kama wao walivyo wamoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hii ndiyo nguvu inayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anasema hakuna umoja pasi na Kristo, kwani Yeye ndiye mhimili mkuu wa usalama na maendeleo ya Kanisa, kazi inayoendelea kutekelezwa na Roho Mtakatifu, ndiyo maana ametumwa ulimwenguni ili kujenga na kuliimarisha Kanisa katika umoja na mapendo unaojidhihirisha katika tofauti za kijamii, watu na tamaduni zao. Kanisa la Kristo linajengwa kwa matofali ya: unyenyekevu, upole, uvumilivu na kuchukuliana katika upendo; mambo ya kawaida kabisa lakini yakizingatiwa yanasaidia kukuza na kuimarisha umoja wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo hija ya maisha ya Yesu Kristo aliyoamua kuifanya, akajinyenyekeza na kuwa mtii hata kufa Msalabani na siku ya tatu akafufuka kutoka katika wafu na hapo akaibuka "kidedea". Wakristo watambue kwamba, kiburi hakina tija wala mashiko katika maisha na utume wa Kanisa. Ramani ya ujenzi wa Kanisa inajionesha kwa namna ya pekee katika matumaini yanayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu na hivyo kuliwezesha Kanisa kudumisha umoja na mshikamano licha ya taofauti msingi zinazoweza kujitokeza kati ya waamini.

Sala ya Yesu kwa ajili ya kuombea umoja wa wafuasi wake na unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu viwasaidie Wakristo kuwa ni mawe hai yenye matumaini hadi siku ile Yesu mwenyewe atakapokuja wakati wa utimilifu wa nyakati!







All the contents on this site are copyrighted ©.