2014-10-24 09:02:02

Askofu mteule Josefu Mlola, tuko pamoja katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu!


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa anapenda kuungana na Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Kigoma, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwajalia kiongozi na mchungaji mkuu wa Jimbo Askofu mteule Josefu Mlola. Hii ni bahati na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wananchi wa Kigoma. RealAudioMP3

Askofu mkuu Rugambwa katika mahojiano maaluma na Radio Vatican anabainisha kwamba, waamini wa Jimbo Katoliki Kigoma kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema Jimboni humo wanapenda wanapenda kutumia raslimali na fursa mbali mbali zilizomo Jimboni Kigoma katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Anasema, umefika wakati kwa waamini wa Jimbo Katoliki la Kigoma kujifunga kibwebwe ili kuwajibika barabara kwa kupambana kufa na kupona na mapungufu au vikwazo vinavyokwamisha mchakato wa maendeleo ya watu kiroho na kimwili Jimboni Kigoma kwa kuwajibika barabara kama ilivyokaziwa wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo Katoliki Kigoma iliyoadhimishwa kunako mwaka 2010 na matunda yake yakatangazwa kunako mwaka 2011.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, waamini wanawajibika katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwa kutumia kikamilifu neema na baraka zinazoendelea kububujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Askofu mkuu Rugambwa ambaye aliwahi kuwa ni Askofu wa Jimbo la Kigoma kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa anapenda pia kuchukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza Askofu mteule Josefu Mlola kwa kukubali na kuitikia wito wa kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, Jimbo Katoliki Kigoma.

Askofu mkuu Rugambwa anapenda kumhakikishia Askofu mteule Josefu Mlola ushirikiano wa dhati kutoka kwa Familia ya Mungu Jimboni Kigoma katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.