Tanzania inaendelea kujinadi kwa walimwengu baada ya kusherehekea miaka 50 ya Uhuru
na Kazi!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amezindua jarida la kimataifa la FIRST ambalo
limesheheni taarifa za kuitangaza Tanzania kwa wadau wa nchi mbalimbali duniani huku
likielezea hatua mbalimbali za ustawi kwa miaka 50 tangu Tanzania ipate ijipatie uhuru
wake kutoka kwa Mwingereza. Uzindusi huo ulifanyika kwenye ofisi za ubalozi wa
Tanzania jijini London, Uingereza ambako pia Waziri Mkuu alikabidhiwa nakala ya kwanza
ya toleo la sasa ambayo iliwekwa kwenye jalada jekundu la ngozi. Akizungumza katika
uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisema Serikali ya Tanzania imepata fursa nzuri ya kujinadi
kwa watu maarufu na wafanyabiashara wa kimataifa duniani kupitia jarida hilo na akataka
uwekwe utaratibu wa kujinadi kisekta. Alimtaka Balozi wa Uingereza, Bw. Peter Kallaghe
aweke mkazo na kusimamia suala hilo ili kuhakikisha matoleo yanayofuata yanakuwa ya
kisekta zaidi. “Balozi hapa umefanya kazi nzuri sana ya kuinadi nchi yetu, wala usichoke.
Tujitahidi sasa kila mwaka waandike kuhusu fursa za uwekezaji kwa miradi ya kisekta
kama utalii, nishati, madini na kadhalika,” alisema. Waziri Mkuu alimshukuru Mwenyekiti
wa taasisi ya First, Bw. Rupert Goodman kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa ajili ya Taifa
la Tanzania. “Kazi uliyoifanya ni nzuri lakini katika tolea lijalo tuangalie jinsi
ya kuitangaza miradi ya uwekezaji ambayo inauzika na iende sekta kwa sekta. Ukisirikiana
na Balozi wetu hapa, lazima utapata kitu kizuri,”alisema. Mapema, akielezea kuhusu
jarida hilo la FIRST, Balozi Kallaghe alisema jarida hilo linasambazwa kwenye mashirika
mbalimbali ya ndege kama vile British Airways, Air Astana, Lufthansa, United Airlines,
Gulf Air, American Airlines, South African Airways, Korean Airways, Etihad Airways,
Qatar Airways na Continental Airlines. “Siyo tu kwamba linasambazwa katika mashirika
haya ya ndege, bali pia linawekwa kwenye vyumba vya kupumzikia (First Class and Business
Class Lounges) abiria wa daraja la kwanza na la pili wa mashirika haya kwenye viwanja
vingi vya ndege,”alisema. Alisema hili ni toleo la sita ambalo limeandaliwa kwa
ushirikiano na ofisi yake (Ubalozi wa Uingereza) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya
Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania lakini pia ikilenga kutangaza fursa za uwekezaji lakini
pia ikitangaza hatua mbalimbali za maendeleo ambazo nchi hii imepitia. Uzinduzi
huo ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba; Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim na Naibu Waziri wa Nishati
na Madini, Bw. Charles Kitwanga. Wengine ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles
Tizeba na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Mwambungu ambao pia wamefuatana na Waziri
Mkuu.