Rais Kikwete kurudi Kijijini kuchunga baada ya kung'atuka kutoka madarakani! Chaki,
Je?
JK: Mfumo wa Rais kung’atuka madarakani ni mzuri. . Unatoa nafasi kwa nchi kupata
mawazo na fikra mpya. . Anaamini Tanzania itapata Rais bora zaidi wa kumrithi yeye. .
Atamani muda wake umalizike akalee wajukuu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa mfumo wa Tanzania ambako Rais anatumikia
nafasi ya uongozi kwa muhula wa miaka mitano na siyo zaidi ya miaka 10 ni mfumo mzuri
na unaovutia kwa sababu unaiwezesha nchi kupata fikra na mawazo mapya.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa anaamini kuwa Tanzania itapata Rais bora zaidi kuliko yeye,
Rais ambaye ataiwezesha Tanzania kusonga mbele kwa kasi kubwa zaidi. Rais Kikwete
pia amesema kuwa anayo hamu kubwa ya kumaliza muda wake wa uongozi, ili arudi kijijini
kushughulika na wajuu wake na mifugo yake.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo,
Jumatano, Oktoba 22, 2014, mjini Beijing, China, wakati akizungumza na mabalozi wa
Afrika wanaoziwakilisha nchi zao katika China. Mkutano huo uliofanyika kwenye Nyumba
ya Kufikia Wageni wa Serikali ya China ya Diaoyutai, ulikuwa shughuli ya kwanza ya
Rais Kikwete katika ziara yake rasmi ya siku sita ya Jamhuri ya Watu wa China ambako
amealikwa na Rais Xi Jinping.
Wakati wa maswali na majibu, Mheshimiwa Balozi
Sola Onadipe, Naibu Balozi wa Nigeria katika China, alishangazwa na kauli ya Rais
Kikwete kuwa anatamani amalize muda wake wa uongozi, ili astaafu na kusema kuwa lingekuwa
jambo la maana kwa Afrika kama viongozi wengine wangekuwa na mawazo ya namna hiyo
ya kuheshimu Katiba za nchi zao na kung’atuka kwenye uongozi muda wao unapowadia.
Rais
Kikwete amemwambia Balozi huyo: ” Ni kweli naona kama muda hauendi kwa kasi ya kutosha,
ili niweze kuwa raia wa kawaida na nipate muda wa kuchunga ng’ombe na mbuzi wangu
na nilime mananasi yangu kwa nafasi ya kutosha. Lakini Mheshimiwa Balozi usishangazwe
na utayari wangu kuondoka katika uongozi.”
“Kwanza utaratibu huu wa miaka mitano
ama miaka 10 ni utaratibu wa Kikatiba, ni jambo lililoko katika Katiba yetu na hatuna
kishawishi cha kulibadilisha. Pili, kazi hii ya Urais ni kazi ngumu sana. Kwa hakika,
binafsi nawaonea gele sana wenye nguvu na ubavu wa kutaka kubakia kwenye kazi hii
kwa miaka mingi. Pengine wana nguvu zaidi kuliko mimi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Lakini
pia kuna uzuri katika mfumo huu wa kwetu kwa sababu kila baada ya miaka mitano na
hata kama ni baada ya kila miaka kumi, anaingia mtu mwingine madarakani akiwa na fikra
mpya na mawazo mapya.” “Mfumo huu ni mfumo unaoniridhisha sana na wala hakuna kinachonishawishi
nibakie katika madaraka zaidi ya muda wangu kikatiba. Nina hakika, nchi yetu itapata
kiongozi mwingine, bora kuliko hata mimi, kuongoza vizuri nchi yetu.”
Rais
Kikwete pia amesema kuwa siyo busara pia kwa kiongozi kuwasikiliza wale wanaoshauri
wakisema kuwa akiondoka madarakani nchi itavurugika. “Kwa hakika, hawa wanatetea maslahi
yao tu wakisema kuwa ukiondoka wewe madarakani, wao hawatakuwa tena mabalozi ama mawaziri
ama nafasi nyingine yoyote.”