Askofu mteule Josefu Mlola kusimikwa rasmi tarehe 26 Oktoba 2014: Tunakuja Kigoma
kuwashika mkono!
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anawaalika
waamini na wananchi wa Kigoma katika ujumla wao kujiandaa kikamilifu pamoja na kuendelea
kusali, ili tukio la kumweka wakfu Askofu mteule Josefu Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma
liende kadiri ya mpango wa Mungu.
Anasema Maaskofu
wanajiandaa kwenda Kigoma ili kumwekea mikono na kumkabidhi Jimbo. Ni siku ya shukrani
kwa Baba Mtakatifu aliyewapatia waamini wa Kigoma mchungaji mkuu, kwa kutambua kwamba,
hadi sasa bado kuna baadhi ya Majimbo Katoliki Tanzania yako wazi na hayajapata wachungaji
wakuu.
Askofu mteule Josefu Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma anatarajiwa kuwekwa
wakfu na hatimaye kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma hapo tarehe 26 Oktoba
2014 Jimboni Kigoma. Taarifa kutoka Jimboni humo inaoesha kwamba, Jumamosi asubuhi
tarehe 25 Oktoba, msafara wa Askofu mteule Mlola utaanza safari kutoka Seminari kuu
ya Kipalapala, Tabora ambako hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Gombera, utume aliouanza
mwaka 2011 baada ya kuhamishwa kutoka Seminari kuu ya Segerea ambako alikuwa ni Gombera
Msaidizi.
Askofu mteule na msafara wake, watapokelewa kwa shangwe na nderemo
na waamini wa Jimbo Katoliki la Kigoma kwenye Kigango cha Usinge, Parokia ya Nguruka
ambayo iko mpakani na Jimbo kuu la Tabora na baadaye watapata chakula cha mchana na
kuendelea na safari yao kuelekea Kigoma.
Askofu mteule atasimama kuwasalimia
waamini watakaokuwa kwenye Chuo cha Newman, ambayo kwa sasa ni Sekondari na kama mipango
itakamilika, basi kinatarajiwa kuwa ni Chuo cha Ualimu. Hiki ni kituo kinachoendeshwa
na Watawa wa Upendo.
Saa 10: 00 Jioni, Askofu mteule Josefu Mlola atatinga
Jimbo Katoliki Kigoma. Saa 12: 00 Jioni atakabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu la Jimbo
Katoliki la Kigoma na baadaye yatafuata masifu ya jioni, ambamo Askofu mteule ataungama
Kanuni ya imani pamoja na kula viapo vya utii wakati atakapokuwa anatekeleza dhamana
yake ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, Jimbo Katoliki la Kigoma
na pote pale atakapotumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kadiri ya mahitaji ya Kanisa.
Masifu yanatarajiwa kuongozwa na Askofu Ludovick Josefu Minde wa Jimbo Katoliki Kahama.
Askofu
mteule Josefu Mlola anatarajiwa kuwekwa wakfu katika Ibada ya Misa takatifu, Jumapili
tarehe 26 Oktoba 2014, tukio ambalo linatarajiwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya Maaskofu
Katoliki Tanzania, viongozi wa Serikali kitaifa na kimkoa pamoja na wageni kutoka
ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Kigoma. Ibada inatarajiwa kuongozwa na Askofu mkuu
Paulo Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Josefu
Mlola alizaliwa tarehe 9 Januari 1966 huko Rombo, Mashati, Kilimanjaro. Baada ya masomo
na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa tarehe 12 Julai 1997. Jimbo Katoliki la
Kigoma, limekuwa wazi tangu tarehe 27 Juni 2012, wakati huo, Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikto XVI alipomteuwa Askofu Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu na kumpatia dhamana
ya kuwa Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika
ya Kimissionari ya Kipapa. Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.