2014-10-22 11:53:41

Wananchi wa Sudan ya Kusini wamechoshwa na vita wanataka amani na utulivu!


Ilikuwa ni tarehe 15 Desemba 2013 Serikali ya Sudan ya Kusini na Wapinzani walipoamua kuweka sahihi mkataba wa amani, ili kusitisha machafuko ya kivita yaliyokuwa yanaendelea nchini humo, lakini kwa bahati mbaya, wananchi wa Sudan ya Kusini waliendelea kuteseka kutokana na ukweli kwamba, viongozi husika, hawakutekeleza makubaliano na matokeo yake walianza kushutumiana kwa kukiuka masharti ya mkataba.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Jumatatu tarehe 20 Oktoba 2014 amewakutanisha ana kwa ana Rais Salva Kiir Mayardit na mpinzani wake Rijeck Machar, ili kuzungumza na hatimaye kutia sahihi kwa mara nyingine tena mkataba wa amani, ili kwa pamoja waweze kuwajibika mbele ya wananchi wa Sudan ya Kusini ambao kwa sasa wamechoshwa na mapigano yasiyokuwa na mashiko wala tija kwa maendeleo na ustawi wa wananchi wa Sudan ya Kusini.

Viongozi hawa kwa pamoja wamekubaliana kushirikiana kwa ajili ya kukoleza tena maendeleo ya wananchi wa Sudan ya Kusini, lengo ambalo SPLM lilisimamia kidete, hadi Sudan ya Kusini ikajipatia uhuru wake Julai mwaka 2011. Majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi kwa ajili ya mafao ya wengi ni kati ya mambo ambayo yataendelea kupewa kipaumbele cha kwanza katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa mjini Arusha chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete ambaye ameonesha mchango wa Tanzania katika mchakato wa upatanisho, haki na amani Barani Afrika.

Mkataba huu ni mwanzo wa njia ndefu katika mchako wa kuhakikisha kwamba, Sudan ya Kusini inaendelea kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu.







All the contents on this site are copyrighted ©.