2014-10-22 07:49:06

Simameni kidete kulinda na kutetea haki za watoto duniani


Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasema kwamba, hivi karibuni, Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF limeonesha kwa kina na mapana juu ya upembuzi yakinifu wa matatizo na changamoto zinazowakabili watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kubainisha mikakati itakayotumika kuwalinda na kuwaendeleza watoto, ili kupunguza vifo vya watoto wadogo.

Ili kufikia lengo hili kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuwekeza katika lishe bora, maji safi na salama pamoja na uhakika wa elimu bora na wala si bora elimu.

UNICEF katika taarifa yake inaonesha kwamba, kuna kundi kubwa la watoto linaloendelea kunyanyasika na kudhulumiwa kwa kutumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu, ngono na picha chafu. Katika miaka ya hivi karibuni, takwimu zinaonesha kwamba, kuna watoto zaidi ya millioni tatu wamefariki dunia katika vita na kinzani za kijamii; watoto millioni sita wamepata umelevu wa kudumu na wengine kujeruhiwa vibaya kutokana na milipuko ya mabomu ya kutegwa ardhini na kwamba, licha ya kampeni ya kimataifa, lakini bado kuna watoto ambao wanalazimishwa kwenda mstari wa mbele, na wengine siku hizi wanatumika katika mashambulizi ya kujitolea mhanga; mambo ya kusikitisha sana!

Askofu mkuu Auza anasema, kuna kundi kubwa la watoto ambao wamefariki dunia kutokana na sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo; kuna watoto wanateseka kutokana na utapiamlo wa kutisha, ukosefu wa makazi na dawa msingi na matokeo yake, watoto hawa wanatumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na mambo yanayo wanyanyasa na kudhalilisha utu na heshima yao. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa na Serikali husika kuhakikisha kwamba, zinazijengea familia uwezo wa kutekeleza dhamana na wajibu wake, hasa wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapofanya kumbu kumbu ya miaka ishirini tangu Mwaka wa Familia Kimataifa ulipoadhimishwa kwa mara ya kwanza.

Wazazi na watoto wafundishwe faida na madhara ya kutumia mitandao ya kijamii; wazazi watekeleze dhamana ya malezi na makuzi kwa ukamilifu zaidi, ili watoto hawa waweze kuwa ni raia wema na wanaowajibika barabara katika ustawi na maendeleo ya Jamii zao.

Askofu mkuu Auza anasema kwamba, Mwezi Novemba, 2014 Jumuiya ya Kimataifa itaadhimisha Kumbu kumbu ya miaka 25 ya Tamko la Haki ya Mtoto Duniani, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza haki msingi za watoto; utu na heshima yao kama binadamu. Watoto wajengewe mazingira mazuri ya maisha, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho na kimwili.

Itakumbukwa kwamba, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kuwapatia chakula, makazi, malazi, elimu na huduma ya afya. Kanisa litaendelea kutekeleza wajibu huu msingi sanjari na kuwasaidia wazazi kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara.








All the contents on this site are copyrighted ©.