Huduma makini kwa watoto wagonjwa ni kielelezo cha upendo wa Kanisa kwa watoto!
Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, Jumanne tarehe 21
Oktoba, 2014 imezindua maabara mpya ambazo zitatumika kwa ajili ya kufanya tafiti
na uchunguzi kwa magonjwa ya watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ni maabara
ambayo ni ya kisasa katika kukabiliana na magonjwa tete yanayowasumbua watoto.
Tukio
hili limehudhuriwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ambaye pia
ni Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù. Maabara hizi zitaweza kutumika na watafiti 150
na kwamba, hadi kukamilika kwake zimegharimu jumla ya Euro millioni 26.
Kardinali
Parolin amewashukuru viongozi na wafanyakazi wa Hospitali ya Bambino Gesù katika jitihada
zaao zinazopania kutoa huduma bora na makini kwa watoto wadogo kutoka sehemu mbali
mbali za dunia, kwa kuwa na tafiti makini zinazotumia vyombo vya kisasa zaidi. Kuna
magonjwa ambayo yanaendelea kuwasumbua watoto, kumbe Hospitali ya Bambino Gesù haina
budi kuhakikisha kwamba, inakuwa na vifaa tiba vitakavyotumika kuwahudumia watoto
wagonjwa na Jamii katika ujumla wake.
Kardinali Parolin anasema, ustaarabu
wa jamii yoyote ile unapimwa kwa kuangilia jinsi ambavyo jamii husika inawajali na
kuwahudumia: wagonjwa, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa
limeendelea kuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma za kijamii, kama kielelezo
cha mshikamano na maskini pamoja na wote wanaohitaji kuonjeshwa huruma na upendo wa
Mungu, kielelezo makini cha imani tendaji, hasa kwa njia ya huduma kwa watoto wagonjwa.
Tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Bambino Gesù, Mababa Watakatifu wamechangia
kwa namna ya pekee katika kuendeleza huduma zinazotolewa na Hospitali ya Bambino Gesù
kama sehemu ya mikakati yao ya shughuli za kichungaji kwa watoto wagonjwa. Hospitali
hii ni kielelezo makini cha huduma ya upendo inayotolewa na Baba Mtakatifu, changamoto
kwa wafanyakazi kuendelea kuwa ni mfano wa kuigwa katika taaluma, ukweli na uwazi;
ukarimu unaozingatia tunu msingi za kiutu na Kikristo pamoja na kujenga mazingira
ambamo kila mtu anajisikia kuwa ni mdau katika kulinda, kutetea na kuendeleza Injili
ya uhai, hata pale sadaka kubwa zaidi inapohitajika.
Hospitali ya Bambino Gesù
haina budi kuendelea kuwa ni kielelezo cha huduma makini kwa watoto wagonjwa pamoja
na familia zao wanaojikabidhi kwa Mtoto Yesu ili kupata tiba ya magonjwa yanayowasumbua.
Anawatakia wadau wote huduma makini pamoja na kujali mahangaiko ya wazazi wanaowahudumia
watoto wao Hospitalini hapo.