Wahamasisheni watu kumkubali, kumpenda na kumwongokea Kristo kwa njia ya ushuhuda
wa maisha yenu!
Maadhimisho ya Siku ya 88 ya Kimissionari Duniani kwa Mwaka 2014 yamepambwa kwa namna
ya pekee na Baba Mtakatifu Francisko kumtangaza Papa Paulo VI kuwa Mwenyeheri, kiongozi
ambaye alijitaabisha kuhakikisha kwamba, Habari Njema ya Wokovu inawafikia watu wa
mataifa.
Ilikuwa ni
siku ya kufunga rasmi maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia, tayari
kuendeleza mchakato wa Mama Kanisa katika azma yake ya kutangaza Injili ya Familia
kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa,
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican
anawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Yesu Kristo ni njia,
ukweli na uzima. Ndiye binadamu aliyekamilika kwani ni Mwana mpendwa wa Mungu, Nafsi
ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Siku ya Kimissionari Duniani inalenga kuwahamasisha
waamini na watu wote wenye mapenzi mema wakubali, wapende na wafurahie kumpokea Yesu
Kristo kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani.
Ni mwaliko na changamoto ya kuachana
na dhambi pamoja na mambo yote yanayosigana na mpango wa Mungu katika hija ya maisha
ya binadamu. Kimsingi watu wanahamasishwa kuachana na dhambi na mambo yote yanamkanganya
mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, ili kumpatia nafasi Yesu Kristo aweze kuwakirimia
neema na baraka katika hija ya maisha yao kwa njia ya Kanisa.
Wakristo watambue
kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanatumwa kutangaza Injili hadi miisho ya
dunia kwa njia ya ushuhuda amini wa maisha yao yanayopata chimbuko lake kwa kukutana
na kutembea pamoja na Yesu katika maisha yao ya kila siku. Wakristo wasaidie kuwafundisha
watu kuyashika mafundisho ya Kristo, ili kweli Injili iweze kupenya na kuleta upya
wa maisha, ili kuweza kumkamilisha mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani.