Papa Francisko kutembelea Uturuki, tarehe 28 - 30 Novemba 2014
Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kufanya hija ya kichungaji nchini Uturuki kuanzia
tarehe 28 hadi tarehe 30 Novemba 2014, kufuatia mwaliko kutoka kwa Rais wa Uturuki,
Patriaki Bartolomeo wa kwanza na Baraza la Maaskofu Katoliki Uturuki. Akiwa nchini
humo atatembelea miji ya Ankara na Istanbul.
Baba Mtakatifu anatarajiwa kuondoka
mjini Vatican, Ijumaa tarehe 28 Novemba 2014 na kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Esemboga, ulioko mjini Ankara majira ya saa 7:00 mchana na hapo atapokelewa
rasmi na atimaye kutembelea Makumbusho ya Ataturk. Atakaribishwa rasmi na baadaye
atafanya mazungumzo ya faragha na Rais kwenye Ikulu pamoja na kuzungumza na viongozi
wa Serikali. Baadaye, Baba Mtakatifu atamtembelea Waziri mkuu wa Uturuki pamoja na
Waziri wa masuala ya kidini nchini humo.
Jumamosi tarehe 29 Novemba 2014 majira
ya saa 3:30 asubuhi, Baba Mtakatifu ataondoka kutoka mjini Ankara kuelekea Istanbul
anakotarajiwa kuwasili saa 4:30. Hapo atatembelea Jumba la Makumbusho la Sofia, Msikiti
mkuu wa Sultan Ahmet pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu
la Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu baadaye atahudhuria Ibada ya Kiekumene kwenye Kanisa
la Kipatriaki la Mtakatifu George na baadaye kukutana kwa faragha na Patriaki Bartolomeo
wa kwanza.
Jumapili tarehe 30 Novemba 2014, Baba Mtakatifu Francisko pamoja
na ujumbe wake, wataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu peke yao na baadaye kufuatia
Liturujia ya Neno itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Kipatriaki la Mtakatifu George.
Hapa viongozi hawa wawili watatoa baraka ya kiekumene pamoja na kutia sahihi tamko
la pamoja. Baba Mtakatifu amealikwa kwa chakula cha mchana na Patriaki Bartolomeo
wa kwanza, hapa Baba Mtakatifu anatarajiwa kutoa hotuba ya shukrani na baadaye jioni
kuondoka kurudi mjini Vatican