2014-10-21 08:50:23

Mshikamano wa upendo kwa watu wote wanaoteseka huko Mashariki ya Kati!


Baba Mtakatifu Francisko siku ya Jumatatu ameongoza kikao cha kawaida cha Makardinali pamoja na viongozi wakuu wa Sekretarieti ya Vatican kuhusu hali ilivyo huko Mashariki ya Kati. Kikao hiki kinafuatia mkutano wa Mabalozi wa Vatican pamoja na Wawakilishi kutoka katika nchi za Mashariki ya Kati, kilichofanyika kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 4 Oktoba 2014.

Mapatriaki kutoka Mashariki ya Kati wamepembua kwa kina na mapana: matatizo na changamoto wanazokumbana nazo wakristo huko Mashariki ya Kati hasa kutoka Iraq, Syria, Misri, Nchi Takatifu, Yordani na Lebanon. Mapatriaki wamegusia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, amani ya kudumu inapatikana huko Mashariki ya Kati, kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho, uhuru wa kidini pamoja na kuziwezesha Jumuiya za Kikristo kutekeleza dhamana na wajibu wake hasa katika sekta ya elimu na afya, ili kujenga kizazi kipya chenye uwezo wa kujadiliana. Wajumbe wamekiri kwamba, mchango wa Jumuiya ya Kimataifa ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha haki, amani na upatanisho huko Mashariki ya Kati.

Kuhusu amani, Makardinali wamesema kwamba, kuna haja kwa Ukanda wa Mashariki ya Kati kubainisha mikakati yake kwa siku za usoni, kwa kutambua kwamba, Yerusalemu kimsingi unapaswa kutambulika kuwa ni "Makao makuu ya Imani" kwa ajili ya dini mbali mbali zilizoko huko Mashariki ya Kati. Hapa Makardinali wanasema, kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba, mgogoro kati ya Israeli na Palestina na ule wa Syria unapata ufumbuzi wa kudumu. Kanisa linalaani mauaji yanayotendwa kwa kisingizio cha udini.

Mababa wa Kanisa wamekazia kwa mara nyingine tena umuhimu wa kulinda na kudumisha uhuru wa kidini na uhuru wa dhamiri kama kielelezo cha utekelezaji wa haki msingi za binadamu. Haki msingi za Wakristo huko Mashariki ya Kati hazina budi kutambuliwa na hasa katika mataifa yale ambayo yanaunganisha siasa na masuala ya kidini.

Wajumbe wamekiri kwamba, kutoweka kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati litakuwa ni kosa kubwa sana kwa Jumuiya ya Kimataifa, kwani uwepo wa Wakristo ni nyenzo msingi katika kuweka uwiano bora hasa katika sekta ya elimu. Hapa Wakristo wanaendelea kuhamasishwa kubaki huko Mashariki ya Kati, licha ya dhuluma na nyanyaso wanazokabiliana nazo siku kwa siku, kwani wanachangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya nchi zao.

Mababa wa Kanisa wameangalia kwa jicho la pekee hali ya Wakristo wanaolazimika kuzikimbia nchi zao na kwamba, wanapaswa kupokelewa na kupata hifadhi katika Makanisa na nchi ambako wanakimbilia ili kusalimisha maisha yao. Hapa pia kuna haja ya kuangalia miundo mbinu ya Ibada ili kukidhi mahitaji ya maisha ya kiroho kwa ajili ya wakimbizi.

Wajumbe wamekubaliana kimsingi kwamba, kuna haja ya kuendelea kupeleka msaada wa hali na mali kwa Jumuiya za Kikristo huko Mashariki kama kielelezo cha upendo na mshikamano na Wakristo hao wanaodhulumiwa na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mshikamano huu unaweza kufanyika kwa njia ya hija za maisha ya kiroho. Elimu inayotolewa isaidie kukuza na kuimarisha uhuru wa kuabudu changamoto ya kuendeleza majadiliano ya kina na Waamini wa dini ya Kiislam sanjari na ushirikiano wa kiekumene.

Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, watu waliokimbia nchi zao kutokana na madhulumu na nyanyaso za kidini wanapata fursa ya kurudi tena katika nchi zao mapema iwezekanavyo. Makardinali wamewataka wale walioteka nyara watu kutoka sehemu mbali mbali huko Mashariki ya Kati kuwaachilia huru mara moja.







All the contents on this site are copyrighted ©.