2014-10-21 10:08:03

Maisha ya Padre Ansovinus Makwanda yamefutika kama ndoto ya mchana kwa ajali ya gari huko Singida!


Maana ya Kikristo ya Fumbo la Kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, ambaye ndani mwake mna tumaini moja katika maisha ya uzima wa milele. Mkristo anayekufa katika Kristo "huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Bwana". RealAudioMP3

Kwa Mkristo siku ya kifo huanzisha, mwisho wa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa kwa Sakramenti ya Ubatizo, kwa kufanana kamili na sura ya Mwana wa Mungu, kulikotolewa kwa mpako wa Roho Mtakatifu, ushirika katika Fumbo la Ekaristi. Maisha ya binadamu yataendelea kubaki kama Fumbo, kwa kutambua kwamba daima binadamu hapa duniani ni msafiri na wala hana makazi ya kudumu!

Katika mkesha wa Siku kuu ya Mtakatifu Gaspar, Muasisi wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Oktoba, Shirika limempoteza Padre Ansovinus Makwanda, kilichotokea Manyoni, Mkoani Singida kwa ajali ya gari. Marehemu Padre Makwanda alizaliwa kunako mwaka 1971 huko Biro, Jimbo Katoliki Mahenge, Tanzania. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu la Ushemasi hapo tarehe 8 Desemba 2001, Jimboni Morogoro. Tarehe 30 Julai 2002 akapadrishwa.

Katika maisha yake amewahi kufanya kazi za kichungaji Parokiani Chibumagwa, Jimbo Katoliki Singida, Mtunza fedha, Seminari kuu ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi Morogoro, Parokia ya Manyoni kama Paroko Msaidizi. Hadi mauti inamfika alikuwa ni Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Kanisa Katoliki Manyoni, Jimbo Katoliki Singida, utume aliokuwa amekabidhiwa na Shirika kuanzia mwaka 2008 ili kuhakikisha kwamba, Shirika kweli linajibu kilio cha damu, kwa kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri kwa njia ya ufundi stadi.

Maisha ya Padre Makwanda yamefutika kama ndoto ya mchana, mwili wake utazikwa ardhini kama mbegu ya mwili utakaofufuliwa katika utukufu! RIP.







All the contents on this site are copyrighted ©.