Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya wanyonge huko Mashariki ya Kati!
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu tarehe 20 Oktoba 2014 katika
kikao maalum cha Baba Mtakatifu na Makardinali kilichokuwa kinajadili kuhusu hali
ilivyo huko Mashariki ya Kati amesema kwamba, hali kama ilivyo kwa sasa ni jambo ambalo
haliwezi kamwe kukubalika na kwamba, wanao wajibu wa kimaadili kukemea kuhusu mateso,
madhulumu na nyanyaso wanazofanyiwa watu huko Mashariki ya Kati. Watu wananyimwa haki
zao msingi na kwamba, zawadi ya maisha, uhuru wa kidini, amani na utulivu vimetoweka
huko Mashariki ya Kati.
Hali ya kisiasa huko Mashariki ya Kati ni tete kiasi
cha kuhatarisha mfungamano wa Jumuiya ya Kimataifa. Mchakato wa amani huko Mashariki
ya Kati hauna budi kuwa ni matunda ya upatanisho wa kitaifa, unaowajumuisha wadau
mbali mbali, ili watu waweze kujifunza kuishi kwa amani, utulivu na mshikamano. Machafuko
ya hali ya kisiasa huko Mashariki ya Kati hayawezi kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa
njia ya mtutu wa bunduki, kwani kuna makampuni makubwa yanayoendelea kujinufaisha
yenyewe kwa kufanya biashara haramu ya silaha katika maeneo ya vita. Jumuiya ya Kimataifa
ina wajibu wa kimaadili wa kukomesha biashara ya silaha huko Mashariki ya Kati inayoendelea
kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Kardinali Parolin anasema kwamba
kuna makundi makubwa ya Wakristo yanayokimbia nchi zao huko Mashariki ya Kati kwa
ajili ya kutafuta usalama wa maisha yao, jambo ambalo wakati mwingine linawatumbukiza
katika mikono ya wafanyabiashara haramu ya binadamu. Inasikitisha kuona Mashariki
ya Kati ikiwa haina tena Wakristo ambao wamekuwepo hapo kwa takribani miaka elfu mbili
huku wakiungama imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.
Wakristo wamekuwa kweli
ni vyombo na wajenzi wa misingi ya amani, upatanisho na maendeleo. Ili Wakristo waweze
kuendelea kuishi huko Mashariki ya Kati, kuna haja ya kuwajengea uwezo wa kuishi katika
mazingira salama, wakiwa na fursa za ajira pamoja na kuwa na mikakati makini ya maendeleo
kwa siku za usoni.
Kanisa kwa upande wake litaendelea kuonesha mshikamano wa
upendo kwa njia ya sala, kwa kuhamasisha majadiliano na upatanisho, ili kweli amani
na utulivu viweze kupatikana tena huko Mashariki ya Kati. Maelfu ya watu yanahitaji
msaada wa hali na mali katika sekta ya elimu, afya na maendeleo, Kanisa hapa linapaswa
kuonesha umoja na ushuhuda wa mapendo. Makanisa mahalia yaendelee kujikita katika
majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga misingi ya haki, amani na utulivu.
Kardinali
Parolin anasema kwamba Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kukaa kimya na kulifumbia macho
matatizo na changamoto zinazojitokeza huko Mashariki ya Kati. Jumuiya hii inayowajibu
wa kimaadili kusitisha vita na watu kuanza kujikita katika majadiliano yanayohimiza
utekelezaji wa haki msingi kwa raia wote, kutafuta mafao ya wengi, kuheshimiana pamoja
na kuthamini mchango unaotolewa na raia wote. Umoja wa Mataifa uhakikishe kwamba,
hakuna mauaji ya kimbari yanayoweza kutokea huko Mashariki ya Kati pamoja na kuwasaidia
Wakimbizi. Jumuiya ya Kimataifa ioneshe mshikamano wa dhati pamoja na kuhakikisha
kwamba, haki inatendeka kwa wote.
Mwishoni, Kardinali Pietro Parolin anasema
kwamba, Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya matumaini kwa wale wote waliovunjika moyo
kwa kushikamana nao katika sala pamoja na kuendelea kuwahimiza kubaki huko Mashariki
ya Kati, kwa kutambua kwamba, wanao mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha mafao,
maendeleo na ustawi wa wengi.