2014-10-21 15:33:13

Jubilee ya Miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu ulimwenguni! Dodoma kuwaka moto hapo mwaka 2015


Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu kila mwaka ifikapo tarehe 21 Oktoba linaadhimisha Siku kuu ya Mwalilishi wa Shirika lao, Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Mtume hodari wa Damu Azizi ya Yesu. Kwa kipindi cha miaka mitatu, Wamissionari hawa wanaendelea na maandalizi ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 200 tangu Mtakatifu Gaspar alipoanzisha Shirika hili ambalo kwa sasa limeenea sehemu mbali mbali za dunia. RealAudioMP3

Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania hapo tarehe 15 Agosti 2015 litakuwa ni Kanda kamili inayojitegemea kwa maisha na utume wake. Kwa sasa Vikarieti ya Tanzania iko chini ya Kanda ya Italia. Padre Eugen Nchimbi atashirikisha zaidi matendo ya Mungu katika maisha yao!

Tarehe 21 Mwezi Oktoba kila mwaka, Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu (yaani C.PP.S) duniani kote tunaadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Mwanzilishi wa Shirika letu, Gaspari Del Bufalo. Katika uhai wake (1786-1837), Gaspari Del Bufalo, kupitia yafuatayo:


Aling’amua kuwa Mungu anawapenda watu wote na ili kuwakomboa alimtoa Mwanaye wa pekee, Yesu Kristo aliyemwaga Damu yake azizi pale Msalabani na anawaalika watu wote kuutambua upendo huo, kugeuza mwenendo wa maisha- kujipatanisha na Mungu; kisha kuwa wajumbe wa upendo huo wa Mungu, kiasi cha kuwafariji wote walio katika mahangaiko ya kimwili na kiroho.

Kwa kuzingatia ucha-Mungu uliodhihirika katika ibada yake kwa Damu ya Ukombozi, mahubiri ya hadharani, ushupavu wake kupitia huduma kwa maskini, huduma kwa wagonjwa na jitihada ya kuwaongoa majambazi; kifo chake cha Desemba 28, 1837 kilifuatiwa na kutambulika kwake, yaani: mwaka 1904 Papa Pio X alimtangaza kuwa Mwenye heri na tarehe 12 Mwezi Juni 1954 alitangazwa na Papa Pio XII kuwa Mtakatifu. Licha ya Papa Pio XII, Mapapa wengine kama vile: Yohane XXIII, Yohane Paulo II, walimtambua kuwa Mtume wa Damu Azizi.

Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu (CPPS) lililoanzishwa na Gaspari Del Bufalo hapo tarehe 15 Agosti 1815 huko Abasia ya Mt. Felix, kijijini Giano, mkoani Umbria nchini Italia, kwa neema ya Mungu limefanikiwa kusambaa kote duniani, limejaliwa wamisionari na wafuasi wengi na mwakani, yaani 2015, litatimiza miaka 200 tangu kuanzishwa kwake.

Ili kujiandaa kuadhimisha vemaJjubilee hiyo, kumefanyika maandalizi ya miaka mitatu ya maandalizi kila mwaka ukiwa na mada ya kutakakari; yaani: 2012/2013: Historia ya Mwanzilishi na ya Shirika; 2013/2014 Karama ya upatanisho na hatimaye, 2014/2015 jitihada za kujibu kwa vitendo kilio cha Damu (mahangaiko ya watu duniani).

Na katika mwaka wenyewe wa Jubilei yaani 2015, matukio mawili yatafanyika nchini Italia yakihudhuriwa na Familia ya Damu Azizi toka duniani kote:


Sanjari na maadhimisho hayo ya kidunia, Wakuu mbalimbali wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi, katika mkutano wao uliofanyika tarehe 13-22 Septemba 2014 huko Dodoma, Tanzania, waliridhia ombi la Vikarieti ya Tanzania kupandishwa hadhi toka Vikarieti kuwa Kanda kamili inayojitegemea. Sherehe ya kuzaliwa kwa Kandai hiyo mpya itaadhimishwa katika kilele cha Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa Shirika, yaani, tarehe 15 Agosti 2015 huko mjini Dodoma, Tanzania.

Hivyo ndivyo ilivyo kwa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Vikarieti ya Tanzania, wakisukumwa na moyo wa umisionari katika kueneza upendo kwa Damu Azizi ya Yesu wakiongozwa na kauli mbiu “ndoto ya Mtakatifu Gaspari inaendelea”, wanawaalika watu wote kusali na kushiriki kwa dhati ili Jubilei hii ituunde upya, vizuri na kwa namna endelevu.

Lengo hilo, linawezakana kwa njia ya Damu ya thamani kubwa ya Bwana wetu Yesu Kristo iliyomwagika kwa ajili ya wokovu wa wengi. Isifiwe na kuabudiwa Damu Azizi ya Kristo, Milele Amina.

Imeandaliwa na
Padre Eugen Nchimbi, C.PP.S.







All the contents on this site are copyrighted ©.