Msishabikie mambo yanayosigana na mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji!
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amewataka
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa waaminifu kwa mpango wa Mungu katika
maisha ya mwanadamu kwa kujikita katika kanuni maadili, huku wakiheshimu maumbile
na kuachana na upuuzi wa walimwengu wanaotaka kushabikia vitendo vya ushoga!
Katika mahojiano
maalum na Radio Vatican, Askofu Ngalalekumtwa anabainisha kwamba, Mababa wa Sinodi
wakati wa maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kuhusu familia wametafakari kwa
kina na mapana baraka ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu kwa kumshirikisha
katika kazi ay uumbaji, inayofanywa ndani ya familia inayoundwa na Bwana na Bibi,
ili waweze kukamilishana na kutakatifuzana katika hija yao ya maisha.
Askofu
Ngalalekumtwa anasema ni mpango wa Mungu kwamba, binadamu aweze kuzaliwa na kupata
malezi na makuzi kutoka ndani ya familia, ili watoto nao waweze kujifunza matendo
makuu ya Mungu kwa njia ya Baba na Mama zao wanaowakirimia mazingira bora ya malezi
na makuzi.
Ushoga ni mambo yanayosigana na mpango wa Mungu katika kazi ya
uumbaji na malezi kwa watoto. Kanisa linatambua ndoa kuwa Sakramenti inayoonesha upendo
wa Kristo kwa Kanisa lake, changamoto kwa binadamu kujikita katika kanuni maadili,
utu wema, nidhamu pamoja na kuheshimu maumbile na kamwe wasipende kushabikia mambo
yanayosigana na mpango wa Mungu.