Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani hapo tarehe
16 Oktoba 2014 amemwandikia ujumbe Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa
Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, akionesha ni kwa jinsi gani
ambavyo baa la njaa linavyotishia amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa na hivyo
kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuibua mbinu mkakati makini utakaozisaidia Jamii za wakulima
vijijini kuzalisha chakula cha kutosha pamoja na kupambana na umaskini.
Baba
Mtakatifu katika ujumbe huo anapenda kuwa ni sauti ya watu wanaoteseka kutokana na
baa la njaa wakati kuna chakula kingi duniani, kinachotupwa kwenye mashimo na mapipa
ya taka, kutokana na ubinafsi unaowasukuma baadhi ya watu kupenda kupata faida kubwa
zaidi.
Baa la njaa ni kati ya majanga makubwa yanayomwandama mwanadamu, lakini
ni janga ambalo bado linaangaliwa kwa "jicho la kengeza" bila kuvaliwa njuga, licha
ya maendeleo makubwa yaliyokwisha kupatikana katika nchi mbali mbali. Serikali nyingi
zimeondoa ruzuku kwa masuala ya kijamii, hali ambayo inaendelea kugumisha maisha ya
watu wengi duniani. Kuna kundi kubwa la watu linalo kabiliwa na baa la njaa na utapiamlo,
ikumbukwe kwamba, hapa binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala si namba.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, haitoshi kutoa msaada kama mbinu ya kupambana na baa
la njaa bali kubadilisha sera na mikakati ya maendeleo, ili kuharakisha mchakato wa
maendeleo kwa kurekebisha sheria na kanuni za Jumuiya ya Kimataifa, ili kujenga na
kuimarisha amani ambayo kwa sasa iko mashakani kutokana na baa la njaa.
Baba
Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Mkurugenzi mkuu wa FAO anabainisha kwamba,
kauli mbiu iliyokuwa imechaguliwa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani
kwa Mwaka 2014: "Familia za Wakulima, Lisheni dunia na tunzeni mazingira" inaonesha
umuhimu wa familia za wakulima vijijini zinavyoweza kushiriki kikamilifu katika mapambano
dhidi ya baa la njaa ikiwa kama zitawezeshwa kikamilifu, kwani wao wanaweza kuchangia
uhakika wa usalama wa chakula duniani pasi na kuharibu mazingira.
Baba Mtakatifu
anasema, ili kufikia lengo hili, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa mahitaji ya mtu mzima: kiroho, kimwili na kijamii na wala si kwa kuangalia
teknolojia peke yake; sanjari na kujenga mshikamano wa upendo na udugu, unaowawezesha
watu kushirikiana na kusaidiana katika kuendeleza gurudumu la maisha ya kijamii.