Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania apongezwa kwa ukarimu kwa wakimbizi kutoka Burundi
Umoja wa Mataifa (UN) umempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete kwa uamuzi wake wa kutoa uraia wa Tanzania kwa waliokuwa wakimbizi
162,156 wa Burundi. Pongezi hizo za UN zimetolewa Alhamisi, Oktoba 16, 2014, na Mjumbe
Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Eneo la Maziwa Makuu, Balozi Said Djinnit
wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete katika Ikulu Ndogo, mjini
Dodoma.
Balozi Djinnit amesema kuwa uamuzi huo wa Rais Kikwete kutoa uraia
kwa mamia ya wakimbizi hao wa Burundi unathibisha na kudumisha tunu za kihistoria
ya ukarimu zaTanzania ambazo zimethibitisha mara kwa mara tokea Uhuru mwaka 1961.
Balozi
Djinnit amemwambia Rais Kikwete: “Nikiwa Mwafrika na Mwakilishi wa Umoja wa Taifa
ni jambo la kufurahisha na kutia matumaini sana kuwa Tanzania inaendelea kuwa mfano
katika kupokea, kuwatunza na hatimaye kutoa uraia kwa wakimbizi. Ni mwendelezo wa
tunu za kudumu za Tanzania.” Ameongeza Balozi Djinnit, “Uamuzi wako huo Mheshimiwa
Rais ambao ni uamuzi wa Tanzania na unakwenda sambamba na tunu za nchi hii ya Tanzania
na pia tunu za Umoja wa Afrika (AU).”
Balozi Djinnit pia amempogeza Rais Kikwete
na uongozi wote wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kupeleka askari wa Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) kujiunga na Jeshi la Umoja wa Mataifa la Force Intervention Brigade
(FIB) la Kulinda Amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). “Ushahidi
uko wazi kuwa Kikosi cha Tanzania ndicho chenye nguvu kubwa zaidi na mchango mkubwa
zaidi katika FIB na tunapongeza na kukushukuru kwa kukubali kutoa askari wa nchi hii
kuingia katika FIB. Vijana wanafanya kazi kubwa na nzuri sana,”.Balozi Djinnit amemwambia
Rais Kikwete.
Aidha, Balozi Djinnit amempongeza Rais Kikwete na Tanzania kwa
kukubali kusuluhisha pande zinazopingana ndani ya chama tawala cha Sudan Kusini cha
Sudanese People’s Liberation Movement (SPLM). Jitihada hizo za usuluhishi ambazo
zinafanywa kichama kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) zimeanza mjini Arusha baada ya
maombi ya chama chenyewe cha SPLM yaliyowasilishwa kwa Rais Kikwete na uongozi wa
chama hicho.
Rais Kikwete amemwambia Balozi Djinnit kuwa Tanzania imeamua kutoa
uraia kwa waliokuwa wakimbizi wa Burundi kwa sababu wametimiza masharti ya kuweza
kuwa raia wa Tanzania, ukiwemo ukweli kuwa wakimbizi hao wamekuwa wameishi Tanzania
kwa miaka 42.
Wakati wa utoaji wa Hati za Uraia kwa raia hao wapya wa Tanzania
katika sherehe iliyofanyika mjini Tabora, Jumanne, Oktoba 14, 2014, Mwakilishi Mkazi
wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR), Mheshimiwa Joyce Mends-Cole alisema
kuwa uamuzi huo wa Tanzania unaifanya Tanzania kuweka rekodi ya kuwa nchi ya kwanza
duniani kutoa uraia kwa kundi kubwa zaidi la wakimbizi na kwa wakati mmoja.