2014-10-16 10:37:09

Msumbiji, kimeeleweka, sasa wanasubiri matokeo!


Tume ya uchaguzi Msumbiji tayari inaendelea kuhesabu kura, baada ya zaidi ya wananchi millioni 10. 9 kupiga kura Jumatano tarehe 15 Oktoba 2014, kwa ajili ya kuwachagua Rais, wabunge 250 na wawakilishi wa Serikali za mitaa 811. Taarifa zinaonesha kwamba, uchaguzi umefanyika katika mazingira ya amani na utulivu. Uchaguzi huu umefanyika miezi miwili tu baada ya Frelimo na Renamo kutiliana sahihi makubaliano ya amani na hivyo kusitisha uhasama wa vyama hivi viwili, uliokuwa umedumu kwa takribani miaka miwili.

Ni matumaini ya wananchi wengi wa Msumbiji kwamba, uchaguzi mkuu wa mwaka huu utasaidia kukata mzizi wa fitina kati ya Frelimo na Renamo, kinzani ambazo zimekwamisha kwa kiasi kikubwa mchakato wa maendeleo ya wananchi wengi wa Msumbiji kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kuanzia mwaka 1975 hadi mwaka 1992.

Wananchi wa Msumbiji wameshiriki katika haki yao ya kidemokrasi kwa kumchagua Rais wa sita baada ya kusitishwa kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe kunako mwaka 1992. Uchaguzi huu umeonesha upinzani mkubwa kati ya wagombea na kwamba, watu wanasubiri kuona matokeo ambayo yataanza kutangazwa na Tume ya uchaguzi Msumbiji zoezi zima la kuhesabu kura litakapokamilika.







All the contents on this site are copyrighted ©.