Mchango wa Paulo VI katika Mafundisho Jamii ya Kanisa!
Mtumishi wa Mungu Giovanni Battista Montini alizaliwa mnamo tarehe 26 Septemba 1897
huko Brescia kaskazini mwa italia. Siku ya kuzaliwa kwake alionekana kuwa dhaifu sana
kiafya, jambo lililo wafanya wakunga waliokuwa wanamsadia mama yake kujifungua kusema
kwamba, mtoto yule angeishi kwa siku moja tu! Alichaguliwa kuliongoza Kanisa kufuatia
kifo cha Baba Mtakatifu Yohane wa XXIII, ambaye kwa sasa ni Mtakatifu kilichotokea
tarehe 3 Juni 1963. Montini aliliongoza Kanisa kuanzia tarehe 30 Juni 1963 hadi tarehe
6 Agosti 1978 kwa jina la Papa Paulo VI.
Mchango wa
Papa Paulo VI unaonekana sana katika mafundisho yake kuhusu jamii yaliyomo kwenye
waraka ” Populorum Progressio” au Maendeleo ya watu”, ambamo anasisitiza kuwepo
uwiano kati ya imani ya kikristo na haki ya kupata maendeleo ya kiuchumi kwa kila
taifa na kwa kila mtu. Katika kuzungumzia maendeleo ya watu “Populorum Progressio”,
Papa Paulo VI anatumia neno “maendeleo” jinsi linavyo eleweka kijamii na kiuchumi,
na anajaribu kulioanisha na uelewa wa kikristo juu ya mwanadamu na jumuiya anaomoishi.
Ana sisitiza kwamba, maendeleo ya watu, na kwa namna ya pekee, hasa maendeleo
ya wale wanao pambana ili kujikomboa kutoka kwenye baa la njaa, maradhi na ukosefu
wa Elimu; wale wanao pambana ili kuweza kupata haki zao msingi katika kushiriki utajiri
ambao Mwenyezi Mungu ameikirimia dunia kwa manufaa ya wote, ni sehemu ya utume na
maisha ya Kanisa.
Barua hii ilitolewa kwenye takriban miaka miwili baada ya
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kipindi ambacho dunia katika ujumla wake ilikuwa
kwenye shamrashamra za aina mbalimbali. Itakumbukwa kwamba, katika kipindi hiki, nchi
nying za Afrika zilikuwa zikijipatia uhuru wa bendera. Kulikuwa pia na mabadiliko
mengi duniani kiuchumi, kisiasa na kijamii. Maendeleo ya sayansi na teknolojia za
mawasiliano yalikuwa yakikua kwa kasi, kiasi cha Umoja wa mataifa kutangaza kwamba
kipindi chote cha kuanzia mwaka 1960 kilikuwa ni kipindi cha maendeleo ( “Decade
of Development”). Si hayo tu, bali pia uchumi ulikuwa unakua kwa kasi pamoja na ushirikiano
wa kibiashara kati ya nchi mbalimbali duniani, jambo ambalo lilionekana kama ndoto
katika historia ya binadamu. Lakini pamoja na maendeleo hayo, kulikuwa na tofauti
kubwa za kiuchumi na kimaisha kati ya watu na watu na kati ya mataifa.
Itakumbukwa
kwamba dunia bado ilikuwa imegawayika katika makundi matatu, au dunia tatu kama inavyojukana.
Dunia ya kwanza ilikuwa inajumuisha nchi za magharibi mwa ulaya pamoja na marekani,
dunia ya pili ikajumuisha nchi za Ulaya ya mashariki, yaani nci za kikomunisti pamoja
na China, na dunia ya tatu ilijumuisha nchi za Afrika, Asia na Amerika ya kusini,
ambazo ziliitwa Nchi maskini na zinazo anza kujipatia maendeleo. Katika ziara zake
za kichungaji Amerika ya kusini na Afrika, Papa Paulo VI aliweza kujionea mwenyewe
umaskini wa hali na mali uliokuwa unawakumba watu wa maeneo aliyotembelea. Hivyo
basi, Waraka wake huu Populorum Progressio una pata chimbuko lake katika uhalisia
wa maisha ya watu, na ndiyo maana anasisitiza kwamba, maendeleo yapanie kumsaidia
mtu mzima kiroho na kimwili.
Hivyo basi, mchango wa Papa Paulo VI katika mafundisho
jamii ya kanisa unaonekana katika msisitizo alio toa kwamba: maendeleo ya kweli ni
yale yanayo muwezesha mwanadamu kujikomboa kutoka katika hali ya umaskini na kumuweka
katika hali ya kuweza kujipatia yeye mwenyewe mahitaji yake yote kwa njia ya kufanya
kazi. Hii ina maanisha kwamba watu wakipewa fursa ya kujiendeleza na kuondokana na
umaskini wataweza kuondokana na hali ya kuishi kwa hofu na kuwa wawajibikaji katika
maisha bila kujisikia kukandamizwa katika jamii. Maendeleo yanayo gusa utu wa mtu
kiroho, kimwili, kiakili na kimahusiano na kimakuzi katika jamii yake ndiyo ambayo
yanaweza kuuthamini utu wa mtu.
Licha ya maendeleo yaliyoletwa na sayansi
na teknolojia za mawasiliano na vyombo vya usafiri, Papa Paulo VI alionya pia kuhusu
hatari ya kusambaratika kwa mila na desturi njema za watu kutokana na uelewa hasi
wa maendeleo. Ilionekana kwamba, kabla ya utandawazi jamii nyingi zilithamini imani,
familia, ushirikiano katika jamii, heshima kwa watu walio pewa dhamana ya kuongoza
jamii na dini za watu. Ila katika ulimwengu ambao unajiita wa kisasa, mambo yote haya
yanaonekana kama kikwazo cha maendeleo, kutokana na tasfiri isiyo sahihih kuhusu maendeleo.
Katika hali hii Papa Paulo VI ana waalika watu watafakari maana ya maendeleo, ambayo
kwake yeye si maendeleo ya vitu bali ni maendeleo ya watu bila kusahau mila na desturi
zao njema.
Kwa wale wanaoungama imani ya kikristo, Papa Paulo VI ana sisitiza
kwamba, maendeleo yaeleweke kupitia imani wanayoiungama, kwani hakuna maendeleo yoyote
yanaweza kupatikana katika kumtenga mwanadamu au mkristo na imani yake, na hata kwa
wale wasio ungama imani yoyote, maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana katika kumtenganisha
mwanadamu na mila na desturi zake au na uchumi wenyewe. Yaani, uchumi ni kwa ajili
ya mwanadamu na si vinginevyo.
Mambo yanapokwenda kinyume na hapo, matokeo
yake ni ukosefu wa haki kati ya watu na watu na pia kati ya mataifa. Ndiyo maana papa
Paoulo VI ana sisitiza kwamba, maendeleo yaliyo ya kweli yanaleta haki na amani katika
jamii na kati ya mataifa, na kwamba mahali ambapo haki inakosekana, hapawezi kuwa
na maendeleo wala amani. Hivyo basi, maendeleo ni namna ya kuleta haki na amani katika
jamii yoyote ile.
Makala haya yameandaliwa na Rev. Dr. Sr. Gisela Upendo
Msuya, mtaalam wa Mafundisho Jamii ya Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu
Thoma wa Akwino, Angelicum, Roma.