Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia, majadiliano ya vikundi yanaendelea!
Mababa wa Sinodi, Jumatatu tarehe 13 Oktoba 2014 walipokea hati elekezi, muhtasari
wa tafakari na mchango uliotolewa na Mababa wa Sinodi wakati wa maadhimisho ya Sinodi
katika juma la kwanza. Hati hii imeendelea kuchambuliwa na Mababa wa Sinodi katika
makundi madogo madogo, ili hatimaye, kuweza kutoa hati ambayo itawakilishwa kwa Baba
Mtakatifu Francisko, ili aweze kuifanyia kazi, mintarafu maadhimisho ya Awamu ya Pili
ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe
4 Hadi tarehe 25 Oktoba 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari, siku ya Jumanne,
tarehe 14 Oktoba 2014, Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican alionesha masikitiko
yake kutokana na tafsiri finyu iliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kiasi hata
cha kupotosha ujumbe uliotolewa na Mababa wa Sinodi katika hati yao elekezi. Mkutano
na waandishi wa habari umehudhuriwa pia na Kardinali Fernando Filoni pamoja na Kardinali
Fox Napier kutoka Afrika ya Kusini.
Mchango unaotolewa na Mababa wa Sinodi
utawasilishwa kwenye kikao cha Sinodi, Alhamisi asubuhi, tarehe 16 Oktoba 2014 na
hapo hati ya Mababa wa Sinodi inatarajiwa kutangazwa rasmi baada ya majadiliano ya
Mababa wa Sinodi katika makundi. Hii hati inajulikana kama "Relatio Synod" ndiyo ambayo
itakayowasilishwa kwa Baba Mtakatifu, tayari kuifanyia kazi kama matunda ya sala na
tafakari kutoka kwa Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia.
Makardinali
hawa wakizungumza na waandishi wa habari wanasema kwamba, majadiliano yanaendelea
na kwamba, Mababa wa Sinodi wanaendelea pia kutoa mapendekezo na ushauri wao katika
tema mbali mbali zilizokwisha kujadiliwa, ili kutoa hati makini kwa Baba Mtakatifu
kwa ajili ya maadhimisho ya awamu ya pili ya Sinodi ya Kawaida ya Maaskofu itakayoadhimishwa
Mwezi Oktoba 2015.