Miaka 15 imekwishagota tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania
alipofariki dunia. Watanzania wanahamasishwa kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa kwa
kujikita katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa
kitaifa, kwa kutambua kwamba, uhuru wa watanzania unawachangamotisha kujitegemea.
Mwalimu Nyerere
alijipambanua kitaifa na kimataifa kama kiongozi aliyesimama kidete kulinda na kutetea
utu na heshima ya binadamu, changamoto endelevu kwa watanzania wakati huu wanapoendelea
kumuenzi. Mwalimu alitaka kuona Tanzania inakuwa na siasa safi na uongozi bora kwani
kwake uongozi ulikuwa ni kielelezo cha huduma.
Katika mahojiano maalum na Radio
Vatican, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,
akiwa mjini Vatican katika Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia anabainisha
mchango uliotolewa na Mwalimu Nyerere katika kupigania uhuru, haki, umoja na mshikamano
wa kitaifa. Ni kiongozi aliyependa kuona watanzania wengi wanashiriki katika ustawi
na maendeleo ya nchi yao kwa kudumisha utawala bora.
Askofu Ngalalekumtwa
anasema mchakato wa Mtumishi wa Mungu Mwalim Nyerere kutangazwa kuwa Mwenyeheri unaendelea
na kwa sasa bado uko katika ngazi ya Kijimbo. Anamwombea kwa Mwenyezi Mungu, ili aweze
kumtakasa na hatimaye, kumkaribisha katika makao ya wenye haki mbinguni.