2014-10-14 07:44:56

"Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi wanaongezeka zaidi duniani"


Taarifa ya Benki ya Dunia inaonesha kwamba, kuna pengo kubwa kati ya watu wachache wenye uwezo kiuchumi na kundi kubwa la maskini, "akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi", hali inayotishia mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na baa la umaskini, njaa na maradhi duniani. Taarifa inaonesha kwamba, ugonjwa wa Ebola kwa sasa ni tishio kubwa kwa usalama wa maisha ya watu duniani, lakini pia hali ya uchumi si shwari sana kwa mataifa mengi.

Benki ya Dunia inazitaka nchi wanachama kuandaa mbinu mkakati utakaobainisha sera makini za kiuchumi zitakazosaidia kupambana na ongezeko kubwa la maskini duniani. Viongozi wakuu wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, kwa pamoja wanasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa jibu makini litakalosaidia kupambana na ugonjwa wa Ebola ambao kwa sasa ni tishio kubwa hata pengine kuliko ugonjwa wa Ukimwi, bila ya kuzitenga nchi zile ambazo zimekumbwa na ugonjwa huu.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa Benki ya Dunia wameridhia kuanzishwa kwa mchakato wa kukusanya fedha itakayosaidia kupunguza pengo kubwa kati ya matajiri na maskini pamoja na kupambana na tatizo la ubaguzi. Ukosefu wa usawa katika masuala ya kijamii ni hatari kubwa kwa maendeleo na ustawi wa Jamii husika. Changamoto hii haina budi kwenda sanjari na maboresho ya huduma ya nishati, afya, maji safi na salama na elimu. Mwelekeo huu hauna budi kujikita katika elimu na mabadiliko ya kijamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.