Mwalimu Nyerere awe ni mfano wa kuigwa katika kusimamia: haki, amani na mshikamano
wa kitaifa!
Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania katika mahojiano
maalum na Radio Vatican, Tanzania inapoadhimisha kumbu kumbu ya kifo cha Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tarehe 14 Oktoba, anawaalika watanzania kumuenzi
Mwalimu kwa kujikita katika misingi ya haki, amani, umoja, mshikamano, utu, heshima
na mafao ya wengi.
Askofu mkuu
Lebulu anasema, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ni kiongozi aliyejipambanua
kwa moyo wa uzalendo, akasimamia haki, amani na mshikamano wa kitaifa. Ni kiongozi
aliyewajali watu wake kiasi hata cha kuyasadaka maisha yake kwa ajili ya ustawi wa
Watanzania na Afrika katika ujumla wake. Kwa Mwalimu uongozi kilikuwa ni kielelezo
cha huduma.
Askofu mkuu Lebulu anawataka watanzania kujibidisha zaidi katika
kushughulikia masuala nyeti na tete yanayowagusa watanzania katika ujumla wao, kwa
kutambua kwamba, kila mtu anawajibika mbele ya Mungu, kwa jinsi gani anavyojitoa kwa
ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wengi, kwa kuweka misingi thabiti ya mustakabali
wa taifa katika masuala ya haki na amani; umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kujenga
taifa linalojipambanua katika Jamii ya kimataifa kwa kusimama kidete kulinda na kutetea
utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Askofu mkuu
Lebulu anakiri wazi kwamba, katika mchakato wa kutunga Katiba Mpya ya Tanzania, nchi
imetikiswa katika msingi wake wa umoja na mshikamano wa kitaifa. Lakini watanzania
wanapaswa kutambua kwamba, kipaumbele cha kwanza hakina budi kutolewa kwa ajili ya
utu na heshima ya binadamu, mafao na maendeleo ya watanzania wote. Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere awe ni mfano wa kuigwa katika kusimamia misingi ya haki, amani,
upendo na mshikamano wa kitaifa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.