Zanzibar-Kejeli na mateso viliwapa imani zaidi kwa Msalaba wa Yesu
Mateso na kejeli za kidini zinazo fanyiwa dhidi ya Wakristo katika visiwa vya Zanzibar,
matukio hayo yamekuwa kichecheo kwa Wakristo, kuimarisha zaidi imani yao na kuona
fahari zaidi Msalaba wa Kristo.Ni ushuhuda ulioonekana katika Parokia ya Mtakatifu
Malaika Mkuu Mikaeli, wakati wa sherehe ya watoto 104, kupokea kwa mara ya kwanza
Ekaristi Takatifu.
Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar, Mhashamu Augustino Shao
ameeleza kuwa, imani ya Kikristo inapigwa vita, makanisa yalichomwa na wengine kuumizwa,lakini
hawajachukua hatua za kulipiza kisasi kwa kuwa kulipa kisasi, si imani ya Kanisa
Katoliki.
Alieleza katika homilia yake, wakati akitoa Sakramenti ya Komunio
ya Kwanza kwa watoto 104 katika Parokia ya Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu, jimboni
Zanzibar, wakati huohuo waamini wa parokia hiyo walipokuwa wanasherehekea sikukuu
ya somo wa parokia hiyo Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu.
Askofu Shao alikumbusha,
miaka miwili iliyopita Kanisa hilo, lilichomwa moto na watu wenye misimamo mikali
ya kiimani, lakini leo hii limesimama upya na watu wa Mungu wanapata nafasi ya kusali
na kuongea na Mungu wao. Ijapokuwa lilichomwa waamini hawakukata tamaa, wameendelea
kushikana mikono na kutembea pamoja kwa upendo. Vijana wengi wanapata sakramenti mbalimbali
za Kanisa kama watoto hao 104, walio pokea Komunio ya Kwanza leo.
Aliendelea
kuwasifu Wakristo hao kwa kushika mafundisho ya Kanisa,akisema, licha ya dhuluma
wanazo fanyiwa kama Wakristo, hakuna mtu aliyeenda kulipiza kisasi na wala hawana
mpango wa kulipiza kisasi, kwani ni kinyume na imani ya Kanisa Katoliki na mafundisho
yake. Aliwatia moyo Wakristo Jimboni mwake akisema, "Kazi yetu ni kusali na kuendeleza
umoja wetu kwani wakati wa matatizo umoja ndio unaosaidia kutatua matatizo mbalimbali.
Tungetengana Kanisa hili lililokuwa limechomwa hapa Mpendae lisingesimama tena.”
Aliendelea
kuwaasa kwamba, uovu hata siku moja hauwezi kutenda wema, waliowachomea Kanisa hilo
mwaka 2012 sasa wanaona aibu na kushangalia ukuu wa Mungu.Wakati wa mateso na kejeli
za kidini, waliweza kupata nguvu zaidi za kuijenga imani katika Msalaba wa Kristo
Msulubiwa.
Amewaasa waamini kuendelea kuwa chombo cha amani katika jamii, kuionyesha
nguvu ya mwanga wa Mungu, kupitia shuhuda za kweli katika maisha na hasa wakati wa
kupambana na changamoto.
“Waamini umoja mliyouonesha wakati wa tabu muuneshe
pia wakati wa raha. Kwa kujenga hili Kanisa upya, mlijinyima mengi hadi leo, hiyo
ndiyo sadaka yenye nguvu na Kristo awatie nguvu,” ameeleza.
Hata hivyo amesema
kuwa, ijapokuwa Kanisa halina malumbano na kazi yake ni kusali kwa ajili ya jamii,
halitasita kukemea na kuonya pale ambapo linaona makosa na upotoshaji unafanyika kwani
kusema ukweli ni wajibu wa Kanisa.
Na akatoa wito kwa waamini kuwaombea viongozi
wa serikali, ili waondokane na ubinafsi hasa wakati huu wa majadiliano ya mchakato
wa Katiba Mpya. Tuwaombee walete katiba inayojenga umoja na amani kati ya jamii yetu,”
ameeleza.
Na aliwaonya waamini wanaopigana na kufarakana kwa ajili ya mchakato
wa katiba kwamba hata kama kuna vipengere visivyo wapendeza au kuwa vya kweli na visivyo
jenga haki, umoja na mshikamano, wawe watulivu wasubiri kukataa wakati wa upigaji
kura.
Katika sherehe hizo vijana waliopata Sakramenti ya Komuniuo ya Kwanza
katika parokia hiyo ni 104, wakiwepo baadhi ya watoto kutoka familia za kiislamu na
kiluteri waliotolewa na wazazi wao kwa nia moja waingie katika imani ya Kanisa Katoliki.
Paroko
wa Parokia hiyo Padri Mushi ameeleza kwamba hata yeye alishangazwa na mtoto mmoja
wa Kiislamu aliyekuja kwake akitaka kubatizwa na kupokea Ekaristi ya kwanza.
“Nilikataa
kwa mara kadhaa lakini wazazi wa watoto hawa walikuja wakisema, Padri watoto hawa
tumeamua wenyewe wawe wakristo katika Kanisa Katoliki. Tumewatoa kwa Kanisa ingawa
sisi ni waislamu. Basi taratibu nyingine za Kanisa zikafuata hadi leo hii wamepata
Sakramenti ya Kumunio ya Kwanza,” ameeleza Padri Mushi.