2014-10-09 16:47:03

Askofu Mkude awataka Mashemasi kutoa huduma bila woga


Mhashamu Telesphor Mkude, wa Jimbo Katoliki la Morogoro Tanzania, hivi karibuni ametoa kwa Daraja Takatifu la ushemasi kwa Mafrateli 22 wa Mashirika mbalimbali ya kitawa, wakati wa Ibada iliyofanyika katika Parokia ya Mungu Mkombozi, ya Chuo Kikuu cha Jordan cha Morogoro. Sherehe iliyohudhuriwa na Wakuu wa Mashirika kutoka nje na ndani ya nchi.

Mwandishi wa habari Immanueli Samweli , anataarifu kupitia gazeti la Kiongozi kwamba, katika sherehe hizo, Askofu Mkude aliwataka Mashemasi kutoa huduma za Kanisa bila woga na kufuata maneno ya Kristo kama kielelezo cha wokovu wa wanadamu wote.

Askofu Mkude, alitaja kazi za Shemasi, kuwa ni pamoja na kusaidia kutoa huduma kwa wagonjwa, kutembelea jumuiya ndogondogo, kutumikia katika Ibada ya Misa Takatifu na huduma zingine zinazohitajika katika kuelimisha jamii. Hivyo hawapaswi kuwa na mipaka wanapotumwa kutoa huduma hizo kwa waamini na kwa jamii inayowazunguka.

Aliwatahadharisha kwamba, wako katika hatua ya mwisho ya kupokea Daraja la Upadri, na hivyo hawapaswi kulichukua daraja hilo kama cheo binafsi , bali wafanye kama Kristo mwenyewe alivyoagiza katika karamu ya mwisho alipokuwa na wafuasi wake, alichukuwa mkate akabariki akisema, ‘Twaeni mle wote huu ndio mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu na kwa ajili ya wote, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” na hapo ndipo wokovu wetu ulipopatikana,” alisema Askofu Mkude.

Na aliwapa pia mfano wa Mtakatifu Yohane wa Msalaba, ambaye siku moja alipokuwa akisali, Mungu alimuuliza, “Unataka tuzo gani kwa kazi ulizofanya na kwa ajili ya mateso uliyoyavumilia? Yeye akajibu, “Tuzo ninaloomba ni kuteswa na kudharauliwa kwa ajili yako.’’ Hivyo Yohane wa Msalaba awe kielelezo cha maisha yenu ya utumishi, ili wote wamjue Mungu na yule aliyemtuma duniani kwa ajili ya ukombozi wetu.

Katika kundi hilo la Mashemasi wapya , mmoja wao Stanslaus Mkombo wa Shirika la OFM Capuchin akitoa ushuhuda alinukuliwa akisema, hatua waliopiga katika Kanisa ni kubwa sana kutokana na juhudi zao katika kusoma kwa bidii na kuzingatia yale wanayofundishwa na Maprofesa wao. Na hivyo alitoa shukurani kwa Maprofesa na sala za waamini kwa kuwasindikiza katika safari yao bila ya kukata tamaa katika masomo ya Falsafa na Teolojia.

Naye Mkuu wa Shirika la Wasalvatoriani Duniani, Padri Millton Zonta ameyashukuru mashirika mbalimbali kwa kuwapeleka vijana wao katika chuo hicho ambacho kipo chini ya Shirika lake na kutoa wito jamii nzima kwamba Chuo Kikuu cha Jordan, kinatoa elimu kwa watu wote wenye dini na wasiokuwa na dini kwani taifa la Mungu si la Kanisa Katoliki pekee yake, bali ni kwa watu wote wenye dini na wasio na dini.
Na Immanuel Samuel-Morogoro








All the contents on this site are copyrighted ©.