Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 27 ya Mwaka A, 5 Oktoba.
Mpendwa, Karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, tugange yaliyomo katika neno hilo
tukiongozwa na nabii Isaya anayetupa ujumbe wa Mungu kwa kielelezo cha shamba la mzabibu,
na kama kawaida Mtume Paulo akiwaandikia Wafilipi anatukumbusha wajibu wa kuhangaikia
zaidi maisha ya sala iliyo njia ya mahusiano na Mungu zaidi ya mambo mengine ambayo
kadiri ya mwinjili Mathayo yaliwafanya Waisraeli wapoteze sifa ya kuwa taifa teule,
sifa ya kuwa shamba la mzabibu, na badala yake Mungu anaanzisha Kanisa, ambalo ni
shamba jipya la mzabibu.
Nabii Isaya anasimulia juu ya shamba la mzabibu jinsi
Bwana alivyo weka bidii na fedha kwa ajili ya kulitunza. Anatarajia matunda mazuri
ya zabibu yenye kuleta faida. Lakini badala yake mizabibu inazaa matunda mwitu! Wale
majirani wa Bwana huyu, walioona uwajibikaji wake, na sifa alizokuwa akitoa kwa shamba
lake la mzabibu, wanaanza kumcheka na kinachofuata ni maskitiko kwake. Akiwa na ghadhabu
kubwa anaamua kuondoa wigo aliokuwa amezungushia shamba hilo.
Mpendwa, huyu
Bwana ni nani na shamba ni nini? Kwa hakika huyu bwana ni Mungu na shamba ndiyo taifa
la Israeli ambalo Mungu alilipenda, alilolizungushia wigo toka utumwani Misri lakini
badala yake limemwacha Bwana na kuzaa matunda mwitu! Mpendwa, hivi leo, sote tu shamba
la mzabibu, tumetengenezwa vema kwa njia ya ubatizo, kipaimara na Ekaristi Takatifu
ndizo neema zake, lakini oneni magugu ya kila aina ndiyo dhambi, magugu yanayoota
katika ulimwengu huu juu ya migongo ya wabatizwa. Hakika tunajiuliza je bado ni shamba
la mizabibu? Nabii Isaya anatualika kuacha kuzalisha magugu zaidi, vinginevyo wigo
uliozungushiwa shamba hili ndizo neema zake utaondolewa kwetu na uzuri wa shamba utapotea
ndiyo kupoteza uzima wa wana wa Mungu.
Mwinjili Mathayo anakazia ujumbe huo
unaoelezwa kwa picha ya shamba la mzabibu, akisema Bwana mmoja mkulima wa mizabibu
amewapangisha wakulima ambao anatarajia wampe malipo yanayomstahili baada ya mavuno.
Lakini badala ya kumpa mastahili yake wanawaua watumishi ambao aliwatuma wakusanye
malipo hayo. Tena mbaya zaidi wanamwua mtoto wa mwenye shamba ambaye alitarajiwa kuheshimiwa
na kuogopwa na watumishi. Jambo hili ni kielelezo cha kukataliwa kwa manabii na hatimaye
Mwana wa Mungu, Masiya mkombozi. Ni mlima wa kiburi cha mwanadamu.
Mpendwa
mwana wa Mungu, jambo hili halikuwa la kawaida na hata hivi leo linatushangaza kwa
Waisraeli kumkataa Masiya. Tena, jambo hili linaonekana kuwa mbali lakini li karibu
kabisa nasi na pengine ndani ya moyo wangu. Namkataa mtoto wa mwenye shamba kwa maana
ya matendo yangu mabaya, kwa maana ya kutojali kwangu katika kuwaheshimu wengine,
tofauti na lile agizo la Mwana anayesisitiza kupendana kama alivyotupenda sisi. Nimeacha
watoto wangu wanataabika kwa kukosa mahitaji ya msingi au hata nimeshindwa kuwajenga
katika tabia njema. Namkataa Mwana kwa kupokea kipaimara kama mtindo wa mavazi ambayo
huja kwa muda tu na kisha kupita! Nakazia jambo hili na hasa mijini, watoto kadhaa
baada ya kupata kipaimara ndiyo mwisho wa kufika kanisani. Kwa bahati, mmoja akifunga
ndoa ndipo tutakutana na baada ya hilo sijui tutakutana naye wapi!
Lipo jambo
jingine ambalo ningependa kukukumbusha tu ili ulitafakari, nalo ni thamani ya Misa
takatifu. Yafaa kuheshimu kina, Misa takatifu katika maisha yako hata kama wengine
watakosa heshima mbele ya Misa takatifu. Kumbuka ni sadaka ya Kristu, ni sadaka ya
msalabani anapojitoa kwa ajili ya ukombozi wako. Hata unapokwenda kuomba Misa uwe
makini, maana mara kadhaa utasikia baadhi ya waamini wakisema Misa shilingi ngapi!
Au nirudishie chenji! Kumbuka Misa huwezi kuinunua na pia unapotoa sadaka, mkono wako
wa kuume usijue mkono wa kushoto umetoa nini. Wengine huthubutu kusema Misa ni yangu,
hapana, ni zawadi ya Kristu kwa ajili ya wote. Kumbe epuka mambo ya chenji na umiliki
wa Misa Takatifu. Vitu hivi vyaweza kuonekana ni vya kawaida lakini polepole vinamengenyua
adili katika maisha ya mwamini. Nimeyataja mambo machache dalili za kumkataa Mwana
wa Mungu, lakini yako mengi mno yafaa uyaangalie na kuyadhibiti mapema ili yasije
yakakutenga na Kristu mkate mtamu wa mbinguni aliyekufanya shamba la mzabibu kwa Damu
yake.
Mtume Paulo anakukumbusha kukazia zaidi mambo ya sala na kuyaacha yale
yanayokuchelewesha kuunganika na Bwana. Anakuomba uweni mtu wa shukrani daima mbele
ya Mungu maana kila ulichonacho ni mali ya Bwana. Kama mmoja atayashika haya amani
ya Mungu ipitayo akili zote itakaa ndani mwake daima. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari
hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya Cpps