2014-10-05 15:58:43

Papa afungua Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili hii 5 Oktoba, 2014, aliongoza Ibada ya Misa Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Vatican, kwa ajili ya kufungua Sinodi Maalum ya Maaskofu juu ya familia. Katika Homilia yake Papa, ametafakari Neno la Mungu kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya kuhusu shamba la Bwana na ndoto yake. Ameeleza Mpango wa Mungu na upendo wake ni kwamba; wakulima watunze shamba la mizabu, kwani mizabibu ni mmea ambao unahitaji huduma.

Papa aliendelea , kwa hiyo ndoto yake Mungu kwa ajili ya watu wake, ni kwamba Yeye anapanda na kulitunza kwa upendo na kwa subira, ili watu wapate kuwa watakatifu na ambao wanaweza kuleta matunda.


Katika unabii wa zamani na katika mafundisho ya Yesu mara nyingi ndoto ya Mungu imesumbuliwa. Kwa sababu katika kitabu cha Isaya inaonyesha kwamba japo shamba la mizabibu lilitunzwa kwa upendo mkuu lakini lilitoa matunda mabichi na yenye uchachu (Is 5,2.4), Wakati Mungu alikuwa anasubiri kupata haki yake, matokeo ilikuwa ni kumwagika damu, alisubiri haki yake, akasikia yowe.


Kwa upande wa Injili Papa anaelezea kwamba ni wakulima ambao waliharibu mpango wa Bwana, wao hawakufanya kazi , bali waliwaza mipango yao inayowahusu.

Katika msemo wa Yesu anawambia wakuu na makuhani, wazee wa watu , kwa maana hiyo wenye busara, ni hao ambao Mungu aliwakabidhi ndoto yake,ya shamba ili walime na kulitunza, isishambuliwe na wanyama mwitu.


Papa alisema , hiyo ndiyo kazi ya wakuu wa watu, kulima shamba la mizabibu kwa uhuru, na kujishughulisha. Yesu anaonyesha kwamba wale wakulima ambao walitawala shamba la mizabibu kwa najivuno na kwa pupa waliamua kuondoa hata uwezekano wa Mungu kukamilisha ndoto yake kwa watu alio wachagua.


Kishawishi cha pupa , Papa aliongeza, kipo daima kwa maana hata katika maelezo ya nabii wa Ezekieli kwa wachungaji, ambao Mtakatifu Agustino aliongelea katika masifu ya jumapili juu ya pupa ya fedha na utawala. Katika kutosheleza pupa hiyo wachungaji wabaya waliwatwisha mizigo mizito isiyochukulika ambayo hata wakuu hao wasingeweza kuinyanyanyua kwa kidole chao(Mt 23,4).


Papa alisema kwamba katika Sinodi ya maaskofu hata wao wanaitwa kufanya kazi katika shamba la mizabibu la Bwana. Mkutano wa Maaskofu siyo wa kujadili mawazo mazuri na ujanja, au kutazama nani mwenye akili zaidi. Lakini ni mikutano kwa lengo la kusaidia kulima na kutunza vema shamba la Bwana, kwa mshikamano wa ndoto yake, kwa ajili ya mpango wake wa upendo juu ya watu wake.

Papa anabainisha kwamba kwa namna hiyo Bwana anawaita kutunza kwa uangalifu familia ambayo tangu asili yake ni sehemu ya ishara yake ya upendo kwa binadamu .


Wote tu wadhambi, aliongeza Papa kwa sababu hata sisi inawezekana tukawa na kishawishi cha kutaka kutawala shamba kwa sababu ya pupa ambayo haikosekani katika maisha ya binadamu.

Ndoto ya Mungu daima inakumbana na unafiki wa watumishi wake, lakini inawezekana kufaidi ndoto ya Mungu iwapo tutaongozwa na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anatupatia busara ambayo ni zaidi ya sayansi, kwa ajili ya kufanya kazi kwa ukarimu na kwa uhuru wa kweli na kwa unyenyekevu kiutendaji.

Papa alimalizia kwa kuwaomba Mababa wa Sinodi, walime na kutunza vema shamba, kwani inabidi mioyo yao na akili zao zijazwe Amani ya Mungu inayozidi akili zote. Wawe ndani ya Yesu kristo kama asemavyo Mtakatifu Paulo Fil 4, 7. Kwa namna hiyo mawazo yao, mipango yao ifananane na ndoto ya Mungu, ili kuunda watu wake watakatifu wanaotoa mtunda ya ufalme wa Mungu (Mt 21,43)








All the contents on this site are copyrighted ©.