2014-08-27 15:51:49

Imani yetu na iwe kioo kinachoonyesha Kanisa Moja na Takatifu


Baba Mtakatifu Francisco, kama kawaida ya mapema siku ya Jumatano alitoa katekesi yake kwa mahujaji na wageni waliokuwa wamekusanyika Vatican. Mafundisho yake, yalizama katika kuelezea nini maana ya kukiri “ninasadiki katika Kanisa Moja na Takatifu “.

Papa alianza, .....Ndugu zangu wapendwa, tunakiri katika sala ya Kanisa, Ninasadiki katika Kanisa moja na Takatifu, kwa sababu asili yake ni katika Utatu Mtakatifu wa Mungu, fumbo la umoja na ushirika kamili. Ni Takatifu kwa sababu limejengwa juu ya Yesu Kristo, na kuhuishwa na Roho wake Mtakatifu, na kujazwa juu yake na upendo wake na wokovu wake. Lakini wakati huohuo ndani mwake mna wadhambi ambao kila siku huanguka katika udhaifu wa dhambi.

Kwa hiyo imani hii tunayokiri, kama waamini wa Kanisa Moja Takatifu , inatusukuma katika kuwa waongofu na ujasiri wa kuishi kila siku katika umoja na utakatifu unaotoka kwa Mungu mwenyewe. Na Yesu Kristo ndiye msingi wetu wa umoja na utakatifu, na hivyo kama sisi kama hatuko katika umoja na kama hatuko watakatifu, basi hatuna imani kwake. Lakini pamoja na udhaifu huo bado hajatuacha peke yetu.

Papa alieleza kuitenga hotuba yake katika vipengere vitatu, akianza na faraja itokayo kwa Mungu kwamba, waamini hupata faraja kutoka kwa Yesu, kwa kuwa tangu mwanzo wa kulijenga kanisa lake aliomba kwa Baba yake, Baba wote wawe na umoja kama wewe Baba ulivyo ndani yangu nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu ,ili ulimwengu upate kusadiki kwamba wewe ndiwe uliyenituma(Yn17; 11.21-23) Papa alieleza na kuongeza kwa njisi gani ilivyo vyema kufahamu kwamba Bwana alitupenda hadi kuyatoa maisha yake kwa ajili ya sisi wenye dhambi, ili tupate mastahili ya kuwa katika umoja huu Mtakatifu. Maneno hayo ya Yesu yanatupa utambuzi kwamba kupitia kwa Yesu pia sisi tunaweza kuingia katika umoja kamili na upendo wake, na katika roho wake , jumuiya za Kristo zinapata dhamana hii kutambuliwa kama jumuiya ya Kikristo zilizo jengwa katika utakatifu.

Papa aliomba umoja wa wafuasi wa Yesu, uliosimikwa zaidi ya yote katika sala ya majitoleo ya mateso na kifo chake msalabani. Kwa ajili hiyo , Papa alitoa mwaliko kwa watu wote kuendelea kutafakari maneno hayo yaliyo andikwa katika Injili ya Yohana 11:21-23 akilitaja kuwa ni neno la ujasiri lililotoka kwa Mungu linalo tuita kila siku katika wogofu. Kupitia kwa Yesu Kristo, ambaye husali kwa ajili yetu na hasa kwa mateso yake,sis wabatizwa kama kanisa lake sote tuungane katika umoja nae na Baba na kati yetu.

Baba Mtakatifu aliendelea kueleza kwa masikitiko kwamba, kwa bahati mbaya , pamoja na kutambua vyema , dhambi ni kinyume cha umoja, wivu na chuki na ubinafsi kuwa kinyume cha usharika, bado tunakaribisha ndani ya roho zetu na katika jumuiya zetu na parokia zetu dhambi hizi badala ya kukumbatia Mapenzi ya Mungu, yanayo tutaka tukuze moyo wa kupendana , kukaribishana na kumpenda kila mtu kama Yesu anavyotupenda sote. Huo ndio utakatifu wa Kanisa , kutambua sura ya Mungu katika mwingine . Hivyo,tunapokiri imani hii katika sala ya Nasadiki, tunahimizwa kujali uongofu wetu , kwa kuwa na ujasiri wa kuishi katika umoja na utakatifu kila siku, kwa utambuzi kwamba unatoka kwa Mungu. Na kwamba, Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyemwilishwa na kuja kukaa kati yetu ni chanzo cha umoja wetu na utakatifu, na kama sisi si wamoja , kama sisi si watu wa Mungu, ni kwa sababu sisi si wafuasi wake. Hata hivyo, Yesu hatutelekezi, bado yu kado akisubiri tumkaribishe tena mioyoni mwetu. Kamwe hawi mbali na kanisa lake.

Na Yesu alitolea sala yake kutoka moyoni kwa Baba yake , akiomba umoja, sisi tunaweza pia sisi kuwa na umoja kati yetu. Na hivyo kwa maneno hayo, Yesu alitenda kama wakili wetu kwa Baba, ili sisi pia tuweze kuingia katika ushirika kamili wa upendo pamoja naye; wakati huo huo, anatoa dhamana kwetu ya kuwa mashahidi wake wa kiroho, na kwa ajili ya utoaji wa majibu mazuri zaidi kwa mtu yeyote ambaye anaye uliza habari ya wokovu na matumaini yetu (cf. 1 Pt 3 , 15).

Papa aliendelea na kipengere cha pili akirejea Injili ya Yohane 17:21: wote wawe kitu kimoja, kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yenu, inaweza wao pia wawe ndani yetu ili ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma. Papa alifafanua Kanisa tangu mwanzo ndivyo lilivyojengwa katika umoja kama yalivyokuwa mapenzi ya Yesu. Na kwamba, Matendo ya Mitume hukumbusha kwamba Wakristo wa kwanza walijulikana kweli kuwa na "moyo huo wa umoja na roho moja" (Matendo 4 , 32); kisha Mtume Paulo aliwahimiza wasishau kuwa "mwili mmoja" (1 Kor 12:13).

Lakini uzoefu wa maisha unatuonyesha kwamba, kuna dhambi nyingi dhidi ya umoja. Na si tu kufikiri juu ya uzushi mkubwa na ukana Mungu, lakini pia tunapaswa kufikiria juu ya mapungufu madogomadogo ambayo tunaweza kuyaita ya kawaida yanayotokea katika jumuiya zetu na hata parokia zetu ambamo washarika wake wameigiwa na dhambi na kusababisha migawanyiko na utengano, inayoletea na dhambi ya wivu, chuki, fitina n.k. Papa anasema, sawa kibindamu tunaona kama ni kawaida lakini si Kikristo! Hii hutokea hasa wakati tukiuweka ubinafsi katika matarajio na ufanikishaji wa malengo ya pamoja. Wengi wetu tunawahukumu wengine vibaya kwa sababu mimi ninataka kufanikisha lililo ndani mwangu kwa kumwangusha mwingine kwa nia mbaya. Wengi tunaangalia makosa ya wengine zaidi yetu tukiyafumbia macho badala ya kutazama ujuzi wao. Mtu anajenga moyo wa kujiona bora zaidi na hivyo kujitenga na mengine na huo ndiyo mwanzo wa migawanyiko inayotokea hata ndani ya jumuiya za kanisa, ambazo zinapaswa kuwa mahali pa kuwaungunisha watu na kuw ana roho moja miongoni wao.

Papa alimalizia na kipengere cha tatu ambamo amezungumzia umuhimu wa kuchunguza dhamiri akisema kwamba, katika jumuiya ya Kikristo, utengano ni moja ya dhambi kubwa zaidi, kwa sababu jumuiya ya Kikristo inapaswa kuwa ishara ya kazi ya Mungu,na si kazi ya shetani. Utengano huharibu mahusiano, na ni mwanzo wa uharibifu kwa jumuiya na chukizo kwa Mungu. Kumbe Jumuiya au parokia vinapaswa kuwa mahali pa kukua uwezo wa kusalimiana yetu, kusamehe na kupendana, kwa kuangalia zaidi na zaidi, ni mahali pa ushirika na upendo. Na hiyo ndiyo maana ya kusali: Nasadiki katika Kanisa Moja na Takatifu. Hii ni kulitambua Kanisa kuwa mfano wa Mungu, lililojazwa huruma yake na neema yake.

Papa alikamilisha mafundisho haya kwa kutoa mwaliko kwa waamini wote , kufanya tafakari ndani ya mioyo yao maneno ya Yesu: "Heri wenye kuleta amani, maana wataitwa wana wa Mungu" (Mt 5,9). Kwa moyo wa dhati, ni kuomba msamaha kwa nyakati zote tunapokuwa na matukio ya kuleta mgawanyiko au kutokuelewana ndani ya jamii zetu, licha ya kuwa na ufahamu kwamba, mgawanyiko huvunja umoja na ushirika katika jumuiya na wala hatuwezi kuendelea kutembea katika njia ya uongofu ulio imara.Na hivyo tumwombe Mungu, ili kwamba mahusiano yetu ya kila siku yaweze kuwa zaidi mazuri na furaha na yenye kutoa mwangwi mzuri katika uhusiano kati yetu na kati yetu a Yesu na katu yetu na Mungu Baba.








All the contents on this site are copyrighted ©.