Shule za Kanisa ni vyombo makini vya Uinjilishaji!
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka
2013 mjini Rio de Janeiro, Brazil aliwakumbusha vijana kwamba wao ni sehemu muhimu
sana ya utume na maisha ya Kanisa, changamoto ya kushiriki kikamilifu katika maisha
ya Kanisa kama wadau wakuu na wala si kama watazamaji.
Huu ni mwaliko
kwa vijana kusimama kidete kulinda, kujenga na kutetea misingi ya haki, amani, upendo,
udugu na mshikamano kati ya watu.
Hili ni jukumu lao na wala hawapaswi kuwasukumia
wengine kulitekeleza. Vijana wanapaswa kuwa ni sehemu ya mabadiliko yanayotafutwa
na Jamii sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu aliwaambia vijana kwamba, wao
ni chombo makini cha Uinjilishaji Mpya miongoni mwa vijana wenzao.
Papa bado
anaendelea kuwaalika vijana kuhakikisha kwamba, wanajitosa kimasomaso kwa ajili ya
kutangaza Injili ya Furaha hadi miisho ya dunia, kwa njia ya ushuhuda makini wa maisha
yao adili na manyofu, hata kwa wale ambao bado hawaguswi na Habari Njema ya Wokovu.
Kuna
uhusiano mkubwa kati ya shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki pamoja
na dhamana ya Uinjilishaji Mpya inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ili kutambua umuhimu huu, kuna haja kwanza kwa walimu,
walezi na wanafunzi wenyewe kufahamu changamoto inayoletwa kwao na Baba Mtakatifu
Francisko.
Shule na taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu vinavyomilikiwa
na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, vimekuwa ni vituo vya majiundo makini ya vijana:
kiakili, kimaadili, kiroho na kiutu, kwa kuzingatia ubora na viwango vya kitaifa na
kimataifa.
Shule, taasisi na vyuo vikuu hivi vimekuwa ni vituo vya majadiliano
ya kidini na kiekumene; mahali pa kurithisha imani, maadili na utu wema. Kutokana
na dhamana hii, Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuwa kweli ni wadau wa Uinjilishaji
Mpya kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yao adili. Jambo msingi kwa walimu,
wazazi na walezi kutambua dhamana na utume wa shule za Kikatoliki katika mchakato
wa Uinjilishaji, ili waweze kushiriki kuwajengea watoto na vijana msingi wa imani,
maadili na utu wema.
Hapa ni mahali pa kujenga na kuimarisha upendo kwa Mungu
na jirani, ili wanafunzi wanaohitimu kutoka katika shule za Kikristo waweze kuwa kweli
ni wadau katika kuyatakatifuza malimwengu. Dunia inawahitaji vijana watakaotoka kifua
mbele kuwatangazia watu Injili ya Furaha, kwa kutambua kwamba, shule na taasisi hizi
ni vyombo makini vya Uinjilishaji Mpya kama ambavyo aliwahi kusema Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto XVI alipokuwa anazungumza na Maaskofu kutoka Marekani wakati wa
hija yao ya kitume mjini Vatican kunako Mwaka 2012.
Hii ni changamoto iliyotolewa
hivi karibuni na Askofu mwandamizi Eamon Martin wa Jimbo kuu la Armagh nchini Ireland.
Anasema, kuna mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi
na maendeleo ya sayansi na teknolojia; mambo ambayo yanaathari zake hata katika sekta
ya elimu. Ukanimungu, ubinafsi, mmong’onyoko wa maadili na utu wema, uhuru usiokuwa
na mipaka ni kati ya mambo yanayoendelea “kupigiwa debe”, lakini matokeo yake ni vijana
wengi wa kizazi kipya kujikatia tamaa na kupoteza mwelekeo wa maisha. Idadi ya vifo
vya vijana wanaojinyonga imeongezeka maradufu kwa miaka ya hivi karibuni.
Kuna
watu wanaojihesabu kuwa ni Wakristo, lakini kwa miaka mingi wamesahau wapi ambako
unapatikana mlango wa Kanisa. Kashfa mbali mbali zilizolikumba Kanisa kwa miaka ya
hivi karibuni zinaweza kuwa zimechangia kwa sehemu kubwa. Kumbe, kuna haja sasa kwa
wadau mbali mbali wa sekta ya elimu kuanzia kwa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba,
wanawajengea vijana wa kizazi kipya mazingira yatakayowasaidia kushiriki kikamilifu
katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, wazazi ni walimu wa kwanza
wa imani kwa watoto wao. Familia ziwe ni shule ya: haki, amani, upendo, mshikamano
wa kidugu na utakatifu wa maisha.
Licha ya mwingiliano mkubwa wa wanafunzi
kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo, lakini wanafunzi wanapaswa
kupewa elimu ya dini au maisha ya kiroho kwani hii ni haki yao msingi. Elimu inayotolewa
na Mama Kanisa anasema Askofu mwandamizi Eamon Martin inamlenga mtu mzima: kiroho
na kimwili na kwamba, Yesu Kristo anatoa maana halisi ya maisha na historia ya binadamu.
Shule, taasisi za elimu na vyuo vikuu vya Kikatoliki havina budi kuendeleza utamaduni
na Mapokeo ya Kanisa kuhusu elimu.
Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Wakristo
kwamba, haitoshi kuwa na jina la Kikristo, bali kutambua kwamba, katika hija ya maisha
wamebahatika kukutana na Yesu ambaye ni dira na kiongozi wao mkuu katika hija ya maisha
yao hapa duniani.
Changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, waamini
wanawatangazia jirani zao Injili ya Furaha kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji,
inayomwilishwa katika matendo adili. Wainjilishaji wawe ni watu wenye furaha inayobubujika
kutoka katika undani wa maisha yao kwa vile wamekutana na Yesu aliyeteswa, akafa na
kufufuka kutoka katika wafu.
Ni mwaliko wa kuwaonjesha wengine upendo na huruma
ya Mungu inayobubujika katika Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti. Kwa hakika
Wakristo wanapaswa kuwa kweli ni chumvi na mwanga wa dunia. Wanahamasishwa kuyatakatifuza
malimwengu. Wawe ni mashahidi wa Imani wanayokiri, adhimisha, mwilisha na kusali,
kama ambavyo inafafanuliwa kwenye Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki.
Wanafunzi
wajengewe utamaduni wa kupenda kusoma na kulitafakari Neno la Mungu ili waweze kusimama
kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu,
yawasukume waamini kuwa kweli ni Wamissionari wa huruma na upendo wa Mungu kati ya
watu wake. Vijana wafundwe kupenda Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kwani hii ndiyo
“injini” ya maisha na utume wa Kanisa. Fumbo la Ekaristi Takatifu liwe ni kiini cha
mshikamano wa upendo na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Watu waguswe na mahangaiko ya jirani zao, tayari kuwaonjesha ukarimu unaobubujika
kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Vyama vya kitume katika shule na taasisi za elimu
vinaweza kuwa ni msaada mkubwa katika ujenzi wa mshikamano na maskini. Kanisa katika
sekta ya elimu, kamwe lisiwasahau watoto wa maskini, ambao wanaweza kubadili na kuboresha
maisha yao kwa njia ya elimu makini.
Askofu mwandamizi Eamon Martin anasema,
kuna haja ya kujenga na kuimarisha uhusiano kati ya: Familia, Shule na Parokia, kwani
makundi haya matatu yanaunda kwa kiasi kikubwa Jopo la Wadau wa Uinjilishaji Mpya.
Watoto na vijana wafundishwe na kurithishwa imani, maadili na utu wema. Waendelezwe
kiakili kwa njia ya elimu makini na kufundwa barabara katika Katekesi.
Mambo
yote haya yataliwezesha Kanisa kuwajengea watoto na vijana uwezo wa kushiriki kikamilifu
katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana wanaweza kushirikisha vipaji na karama zao,
furaha na matumaini yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Shule za Kikatoliki ni
chanda na pete katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya.
Taarifa hii imehaririwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.