2014-08-23 09:37:14

Jielekezeni zaidi katika kujibu wito wenu wa maisha ya kitawa!


Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Canada mwaka 2014 linafanya kumbu kumbu ya miaka 60 tangu lilipoanzishwa, changamoto kubwa iliyoko mbele ya watawa kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya za kitawa zinajielekeza zaidi katika kujibu wito wao wa kukutana na Mwenyezi Mungu, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa njia ya ushuhuda wa huduma makini zinazotolewa na watawa katika Kanisa na Jamii kwa ujumla. RealAudioMP3

Shirikisho hili linaadhimisha kumbu kumbu hii, wakati Mama Kanisa anajiandaa kuadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani utakazozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2014. Katika ujumbe wake kwa wakuu wa Mashirika, Askofu mkuu Paul –Andrè Durocher, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, CCCB anawahimiza watawa kuwa ni vyombo makini vya Uinjilishaji Mpya kwa kujikita katika wongofu wa shughuli za kichungaji pamoja na kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014.

Katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya mambo makuu yafutayo yanapewa kipaumbele cha kwanza kwa Familia ya Mungu nchini Canada. Jambo la kwanza ni ushuhuda unaojikita katika maisha ya kijumuiya kama watu waliokutana na Yesu katika hija ya maisha yao, wakaacha yote na kuamua kumfuasa kama ilivyokuwa kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo. Hii ni Jumuiya ya Waamini inayojisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani.

Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanapaswa kumwilisha karama za Mashirika yao kama kielelezo makini cha ushuhuda wao kwa Kanisa mahalia. Jumuiya za Kitawa ziwe ni kielelezo cha huduma inayofanywa kwa Jamii kwa kuondokana kabisa na chachu ya ubinafsi unaoweza hata kujionesha kwa njia ya Mashirika ya kitawa na Kazi za kitume.

Mashirika yote yanahamasishwa kushirikiana kwa pamoja kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa mahalia, kwa kuwasaidia watu kumwendelea Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa, ili kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika msingi wa haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Mashirika ya kitawa yawe ni chachu ya hija ya upatanisho, matumaini, uponyaji na upyaisho wa maisha ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko ana matumaini makubwa kwa watawa kwamba, watachangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya dhamana ya Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Watawa washiriki katika maisha na utume wa familia kwa kuwasaidia wanandoa na familia katika maisha ya kiroho na kimwili kwa njia ya sala, mafungo, kazi na mashauri mbali mbali. Watawa wajitambue kwamba, hata wao ni sehemu na matunda ya familia ya Kikristo, wanaopaswa kushuhudia tunu msingi za maisha ya kifamilia kwa njia ya maisha ya kijumuiya ndani ya mashirika yao, kwa njia ya huduma inayoonesha ile furaha ya ndani kwa kuongozwa na moyo, ari na upendo kwa njia ya huduma.

Watawa wanapaswa kushirikiana na Maaskofu mahalia kama inavyobainishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika ile hati ya Upendo Mkamilifu. Watawa washiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, pamoja na kuendelea kulisaidia Kanisa kuonesha ule umuhimu wa kuwa kweli ni Familia ya Mungu inayowajibika. Watawa waoneshe kwamba, wao ni Jumuiya ya waamini, inayojikita katika imani, upendo wa kidugu, huruma na unyenyekevu.
Imehaririwa
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.