2014-08-23 11:34:12

Familia ni chachu ya maendeleo endelevu!


Jamii haina budi kujikita katika huduma kwa familia kwa kutumia akili, ujasiri na upendo, mambo msingi katika mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa, itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 27 Septemba 2015. Inahitajika akili kuweza kusoma alama za nyakati kwa kutambua fursa, changamoto na matatizo yanayozikabili familia kwa nyakati hizi.

Kunahitajika ujasiri wa kuweza kusimama kidete kukabiliana na changamoto na matatizo katika familia pasi ya kukata wala kukatishwa tamaa. Kunahitajika upendo wa dhati, ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Familia inayojikita katika Injili ya Uhai. Ni ufafanuzi uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia katika uzinduzi wa maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa, yatakatofanyika Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani.

Maandalizi ya maadhimisho haya hayana budi kujikita katika taalimungu ya familia, tasaufi na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, uelewa wa Kanisa na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya ndoa na familia kadiri ya mafundisho ya Kanisa Katoliki. Kuna haja ya kuangalia pia mada pacha kama vile familia na changamoto za uhamiaji; familia na majadiliano ya kidini na kiekumene.

Mambo yote haya yanahitaji anasema Askofu mkuu Paglia kusindikizwa kwa jicho la akili, ujasiri na upendo kwa familia, kwani familia ni msingi wa maisha na utume wa Kanisa kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko. Ukweli huu unajidhihirisha kwa Baba Mtakatifu kuitisha Sinodi za Maaskofu katika awamu kuu mbili, ili kuzungumzia kwa kina na mapana na hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya utangazaji wa Injili ya Familia inayojikita katika Injili ya Uhai.

Kumbe, si haba kwamba, katika maadhimisho ya Sinodi zote mbili, hapo kati kati kuna maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa. Ikumbukwe kwamba, hata Umoja wa Mataifa unatambua umuhimu wa familia katika mchakato wa maendeleo endelevu ndiyo maana Umoja wa Mataifa unaendelea kuwaalika wadau mbali mbali kushiriki kikamilifu katika maboresho ya familia ya binadamu sehemu mbali mbali duniani. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kukazia umoja, upendo na mshikamano wa dhati, ili kwa pamoja waweze kushirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu.

Ikumbukwe kwamba, familia ni kikolezo kikuu cha maendeleo endelevu ya binadamu, hivyo kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu, ili kuweza kujenga Jamii inayowajibika na kushuhudia uzuri wa Injili ya Familia duniani.
Imehaririwa na
Padre RichardA. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.