2014-08-22 14:54:23

Wazazi wa Marehemu James Foley waguswa na faraja kutoka kwa Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko, Siku ya Alhamisi, tarehe 21 Agosti 2014, amewapigia simu na kuzungumza na Bwana na Bibi John na Diane Foley, wazazi wa mwandishi wa habari kutoka Marekani James Foley aliyeuwawa kikatili kwa kukatwa kichwa na Jeshi la Jihadi, huko Iraq hivi karibuni.

Akizungumza na Radio Vatican, Padre Ciro Benedettini, Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Habari ya Vatican anasema kwamba, Baba Mtakatifu aliweza kuongea na wazazi wa mwandishi huyu wa habari na kuwafariji kutokana na msiba huu mkubwa ambao umewagusa na kutikisa maisha yao.

Baba Mtakatifu ameshangazwa na imani thabiti iliyooneshwa na Mama yake Marehemu James Foley, licha ya majonzi makubwa aliyokuwa nayo. Baba Mtakatifu amewafariji wote na anatumaini kwamba, tukio la kikatili namna hii halitaweza kurudiwa tena.

Wazazi wa Foley wanaishi huko Richmond katika eneo la Hampshire, wameshangazwa kupokea simu kutoka kwa Baba Mtakatifu mwenyewe na wamemshukuru kwa kuonesha ukaribu wake katika mateso na mahangaiko yao kwa kuondokewa na kijana wao. James Foley, 40 alisoma katika Chuo Kikuu cha Marquette, kinachomilikiwa na kuendeshwa na Wayesusit, huko Wiconsin. Licha ya kazi zake zilizomfanya kuhamahama, lakini aliendelea kuwasiliana na wazazi wake mara kwa mara na daima aliwaomba kumsindikiza katika utume na maisha yake kwa njia ya sala.

Alipenda kusali Rozari takatifu hata wakati wa shida na mahangaiko nchini Lybia na Syria kunako mwaka 2012 alipata faraja kwa kumkimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Mama Foley anasema anajivunia kuwa na kijana mwenye ujasiri, aliyethubutu kujisadaka kwa ajili ya kuwashirikisha walimwengu mateso na mahangaiko ya wananchi wa Iraq. Mama huyu anawataka wanajeshi wa Jihadi kuachana na ukatili wao kwa kusalimisha maisha ya watu ambao wamewateka nyara.

Tarehe 26 Agosti 2014, Chuo kikuu cha Marquette kimeandaa sala maalum kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu James Foley. Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican amekazia umuhimu wa kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko katika kuwafariji wazazi wa James Foley, ni kusaidia kuponya madonda ya ndani kwa kuomba faraja na huruma ya Mungu.

Itakumbukwa kwamba, Familia ya Bwana John na Diane Foley, Jumatano tarehe 20 Agosti walipata pia simu kutoka kwa Rais Barack Obama wa Marekani aliyewapigia ili kuwafariji kutokana na kuondokewa na kijana wao James Foley.







All the contents on this site are copyrighted ©.