2014-08-22 08:49:55

Waelimisheni watu juu ya utunzaji bora wa mazingira!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika maadhimisho ya Siku ya utunzaji bora wa mazingira kitaifa inayoadhimishwa hapo tarehe 1 Septemba 2014 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Elimisha juu ya utunzaji bora wa mazingira, kwa ajili ya ustawi wa nchi na miji yetu”. RealAudioMP3

Uchafuzi wa mazingira ni hali ambayo inaendelea kuhatarisha maisha ya viumbe hai ndani na nje ya Italia, kiasi hata cha kuharibu agano kati ya Mwenyezi Mungu na viumbe wake. Watu wamegeuka kuwa ni waharibifu wakubwa wa mazingira, kiasi kwamba, damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika siku hadi siku; watu wameshikwa na hofu kutokana na matumizi ya nguvu.

Licha ya mambo yote haya, lakini Mwenyezi Mungu ameendelea kuwa mwaminifu kwa agano lake, kama yanavyoonesha Maandiko Matakatifu, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa udugu sanjari na kutunza uzuri wa kazi ya uumbaji na vyote vilivyomo. Tangu mwanzo Mwenyezi Mungu aliumba bustani nzuri akampatia mwanadamu kuitunza na kuiendeleza. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji, Injili ya Furaha anasema kwamba, mwanadamu amepewa dhamana ya kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya viumbe wengine pia.

Uharibifu wa mazingira ni kosa ambalo linafanywa na binadamu, kumbe kuna haja ya kujutia kosa hili, kwa kuhakikisha kwamba, mwanadamu anajitahidi kutunza mazingira ili kwamba, pale anapopitia pasibaki kuwa ni nyayo za uharibifu na kifo, mambo yatakayoathiri hata kizazi kijacho.

Bustani ambayo imeharibiwa ni kielelezo cha kumong’onyoka kwa maadili na utu wema, mambo yanayojionesha ndani na nje ya maisha ya mwanadamu. Tatizo kubwa linalomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo ni uchafuzi mkubwa wa mazingira unaosababishwa na uchu wa mali na faida kubwa, hali inayosababisha watu kuwa na matumizi mabaya ya mazingira, kiasi kwamba, uchafuzi huu umekuwa ni chanzo cha magonjwa kama vile Saratani. Watu hawasutwi na dhamiri nyofu na wanaona kana kwamba, yote ni sawa tu! Lakini kuna haja kwa watu kubadilisha mtindo na mfumo wa maisha.

Mafuriko na matetemeko ya ardhi yamekuwa ni chanzo kikuu cha vifo na uharibifu mkubwa wa makazi ya watu na miundo mbinu, kiasi kwamba, waathirika wanapofikwa na majanga haya, kunakuwepo na mshikamano wa hisia bila hata kugusa undani wa mtu. Watu wanafahamu vyanzo vya majanga haya lakini bado wanaonesha mioyo migumu, hawataki kubadilika.

Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kuzuia majanga, kuliko mtindo wa sasa kuanza kushughulikia majanga baada ya kuona athari zake. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Injili ya Furaha anawaalika watu kutaabikiana na kusaidiana kwa hali na mali, kama kielelezo cha upendo na mshikamano wa kidugu.

Changamato kubwa kwa sasa ni kuelimisha dhamiri nyofu kwa kila mtu kwani utunzaji bora wa mazingira ni dhamana ya wote. Kazi ya kurithisha dhamana hii ifanywe kuanzia shuleni kwani mazingira bora ni chanzo cha matumaini hata katika sekta nyingine kama vile: kilimo, utalii na maendeleo endelevu. Sera na mikakati ya uchumi isaidie kuwa na matumizi bora ya ardhi, kwa kutengeneza fursa za ajira pasi na kuharibu mazingira. Katekesi makini isaidie juhudi hizi miongoni mwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema.

Umefika wakati wa vyombo vinavyohusika na utunzaji bora wa mazingira kuwashughulikia watu wanaoharibu mazingira kisheria. Wananchi wawajibike kulinda na kutunza mazingira kwani ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao. Wale wanaochafua mazingira walipe fidia kutokana na uharibifu huu. Lakini yote haya yanaweza kufanikiswa ikiwa kama kutakuwepo na mshikamano wa dhati kati ya watu ndani ya Jamii.

Kila mtu ajisikie kuwa ni sehemu ya utunzaji bora wa mazingira na wala si mtazamaji kama inavyojionesha kwa watu wengi wa nyakati hizi. Watu wawe na ujasiri wa kubadili mfumo na mitindo ya maisha, kwa kuwa na matumizi ya kiasi, ili kupunguza uchafuzi na uharibifu wa mazingira. Ikumbukwe kwamba, mazingira bora ni chanzo kikuu cha fursa za ajira kwa vijana. Vijana wasimame kidete kulinda na kutetea mazingira.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.