Utajiri wa mafuta kutoka Uwanda wa Delta Nigeria unaweza kuwa ni chanzo cha majanga
ya kitaifa!
Askofu Lucius Ugorji wa Jimbo katoliki Umuahia, nchini Nigeria anasema kwamba, utajiri
mkubwa wa mafuta ulioko kwenye Uwanda wa Delta, Nchini Nigeria unaweza kuwa ni chanzo
cha majanga na uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu nchini Nigeria, ikiwa
kama haki na utawala wa sheria havitazingatiwa. Askofu Ugorji ameyasema hayo hivi
karibuni alipokuwa anazungumza katika semina ya siku moja ya wawekezaji wakuu katika
Uwanda wa Delta.
Askofu Ugorji amepembua kwa kina na mapana mambo mbali mbali
yanayoashiria ukosefu wa uongozi bora na utawala wa sheria katika eneo hili ambalo
lina utajiri mkubwa wa mafuta ambayo yamekuwa pia ni chanzo cha kinzani na migogoro
ya kijamii.
Kuna kiasi kikubwa cha fedha inayozalishwa katika eneo hili, lakini
fedha hii inatakatishwa na wajanja wachache na kuingizwa tena kwenye mfumo wa biashara.
Kuna baadhi ya watu binafsi na makundi ya watu yanayotaka kubinafisha uzalishaji wa
mafuta ghafi kutoka Uwanda wa Delta, madhara yake yanaweza kuwa ni makubwa kwa wananchi
wa Nigeria kwani hiki kinaweza kuwa ni chanzo cha uvunjifu wa amani na utulivu nchini
Nigeria.
Askofu Lucius Ugorji anahoji, Je, inawezekana vipi kudhibiti uzalishaji
wa mafuta ghafi, ili usiwe ni chanzo cha majanga nchini Nigeria? Je, haiwezekani kabisa
kwamba, fedha inayozalishwa katika ukanda huu ikatumika kwa ajili ya kugharimia kampeni
za chaguzi mbali mbali nchini Nigeria na matokeo yake, watu hawa wakiishakuingia madarakani
wanalazimika kutekeleza matakwa ya wafadhili wao wakati wa Kampeni za uchaguzi.
Bado
kuna ufisadi na wizi mkubwa wa mali ya umma kwenye Uwanda wa Delta mambo ambayo yanapaswa
kudhibitiwa na Serikali kwa kuzingatia utawala wa sheria na kanuni maadili, daima
mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza. Kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira katika
eneo hili kutokana na kuvuja kwa mafuta katika mkondo wa maji, mambo yanayofanywa
wakati mwingine kwa njia ya hujuma. Mambo yote haya ni tishio kubwa katika utunzaji
bora wa mazingira.